NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Serikali imeelekeza taasisi za udhibiti wa biashara nchini kuboresha mifumo ya utekelezaji wa viwango, usalama wa bidhaa na utoaji wa taarifa sahihi kwa walaji, kwa lengo la kuimarisha ulinzi wao na kuhakikisha ubora wa bidhaa sokoni.
Maelekezo hayo yametolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, Aprili 2, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Haki za Mlaji Duniani 2026.
Kapinga ameitaka Tume ya Ushindani (FCC) pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha wanaboresha mifumo yao kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya ushindani, ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika soko.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mifumo madhubuti ya kupokea na kushughulikia malalamiko ya walaji kwa wakati, hatua itakayosaidia kuongeza imani ya wananchi kwa taasisi hizo.
Amesema mlaji ni mhimili muhimu katika ukuaji wa uchumi wa taifa, hivyo ni wajibu wa FCC kuhakikisha analindwa ipasavyo, hasa baada ya serikali kuipa mamlaka ya kisheria ya kushughulikia malalamiko ambayo hapo awali yalikuwa chini ya mahakama.
Pia ameitaka tume hiyo kuhakikisha maadhimisho yajayo yanahusisha zaidi wadau mbalimbali, wakiwemo walaji, ili kuongeza uelewa wa haki zao na kuimarisha ushirikiano kati ya pande husika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa FCC, Aggrey Mlimuka, amesema tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ya kulinda walaji kwa kushughulikia malalamiko na kuhakikisha wanapata bidhaa zilizo salama na zenye viwango vinavyokubalika.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema bado kuna changamoto ya uelewa mdogo wa haki za mlaji miongoni mwa wananchi, huku akibainisha kuwa juhudi za utoaji elimu kwa umma zinaendelea ili kuwasaidia walaji kufanya maamuzi sahihi.
Katika hatua nyingine, FCC imeendesha kampeni za elimu katika mikoa ya Dar es Salaam na Njombe ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua uelewa wa masuala ya ushindani wa kibiashara na haki za mlaji nchini.

No comments:
Post a Comment