Na Mwandishi Wetu Kibaha, Pwani
Serikali kupitia mradi wa Uendelezaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaosimamiwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 19.8 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu mikubwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani.
Miradi hiyo inahusisha ujenzi wa Soko la Kisasa la Mnarani, barabara mbili zenye urefu wa Kilomita 4.8 kwa kiwango cha lami, Bustani ya Mapumziko na Burudani pamoja na ujenzi wa jengo la Usimamizi wa Mradi.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kuongeza fursa za ajira, kuchochea ukuaji wa uchumi, kuboresha hali za biashara, kuboresha huduma za usafiri na usafirishaji, kupendezesha mji na kuongeza mapato ya Halmashauri.
"Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea mradi huu, ukikamilika tunaenda kukusanya mapato yasiyopungua shilingi milioni 400 ambapo bajeti yetu itakwenda kupanda mpaka shilingi Bilioni 18. Nitoe wito kwa wananchi wa Kibaha kuitunza miundombinu hii pindi itakapokamilika", amesema.
Naye, Mratibu wa mradi wa TACTIC Manispaa ya Kibaha, Mhandisi John Alexander ameeleza mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara za Tughe-Anglikana (Km 1.1) kata ya Tumbi, Barabara ya Picha ya ndege- Hospitali ya Lulanzi-NDC (Km 3.7) inayounganisha kata ya Picha ya ndege na Tangini na ujenzi wa Soko la Mnarani ambapo chanzo cha fedha ni mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.
Kwa upande wake, Mhandisi Fredrick Nzogela kutoka TARURA wilaya ya Kibaha, amesema kupitia mradi huo mtandao wa barabara za lami unaosimamiwa na TARURA utaongezeka kutoka Km 39 hadi kufikia Km 43 ambapo kutakuwa na mitaro ya maji ya mvua itakayosaidia kuondoa maji na taa za barabarani zitakazosaidia biashara kufanyika hadi usiku.
Naye, Diwani wa kata ya Picha ya Ndege, Mhe. Grace Jungulu ameishukuru serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa barabara ya Picha ya ndege-Hospitali ya Lulanzi-NDC itakayosaidia wagonjwa kufika hospitali ya wilaya ya Lulanzi bila changamoto na pia itasaidia wananchi kufanya biashara zao na kufika soko la Mnarani kwa urahisi.
Bw. George Mode, Mwenyekiti wa mtaa wa Mkoani A kata ya Tumbi amesema ujenzi wa barabara ya Tughe-Anglikana italeta tija kwa wananchi kufika kwa urahisi hospitali ya Tumbi na pia itatumika kama "bypass" kwenda Picha ya Ndege na kupunguza foleni ya barabara kuu ya Morogoro.
Naye, mfanyabiashara katika soko la Mnarani, Bi. Amina Mwinyimvua amesema wafanyabiashara wameupokea kwa mikono miwili mradi huo ambapo ameomba soko litakapokamilika wapewe kipaumbele kuendelea na biashara zao.







No comments:
Post a Comment