Serikali ya Tanzania imeungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Maji Duniani, tukio hili muhimu la kimataifa hufanyika kila mwaka tarehe 22 Machi. Mwaka huu maadhimisho haya yalibeba kaulimbiu isemayo “Maji na Jinsia”, iliyolenga kuangazia uhusiano wa karibu kati ya upatikanaji wa huduma ya maji na usawa wa kijinsia.
Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa kujumuisha ukubwa wa jamii na makundi yote katika usimamizi wa rasilimali za maji pamoja na katika ngazi zote za maamuzi katika kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa maendeleo ya jamii.
Nchini Tanzania, kuelekea siku ya maji Duniani, yapo mengi yaliyofanyika kuhusiana na Sekta ya Maji ikiwamo Mkutano wa Pamoja wa Mapitio ya Sekta ya Maji (Joint Water Sector Review), ambapo wadau kutoka sekta mbalimbali walikutana kujadili mafanikio, changamoto na mustakabali wa Sekta ya Maji nchini katika kuimarisha huduma hiyo. Kusanyiko hilo ni jukwaa lililowakutanisha watunga sera, wataalamu, washirika wa maendeleo na wawakilishi wa jamii ili kwa pamoja kuchangia maendeleo ya sekta hiyo muhimu.
Mkutano huo ulikuwa na lengo mahsusi la kupitia utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Tatu (WSDP III) kwa kipindi cha Januari hadi Desemba 2025. Kupitia majadiliano hayo, wadau walipata fursa ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, kubaini changamoto zilizojitokeza, na kuweka mikakati madhubuti ya kuzitatua na kuwa na majibu kamili kwa wananchi.
Moja ya nyaraka iliyopitiwa na kujadiliwa ilikuwa ni Taarifa ya Sekta ya Maji ya mwaka 2025, ambayo ilielezea kwa kina maendeleo yaliyopatikana katika maeneo mbalimbali. Taarifa hiyo ilihusisha usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji, ubora wa maji, pamoja na utoaji wa huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Aidha, iligusa maeneo muhimu kama uratibu wa fedha, sera na mipango, ufuatiliaji na tathmini, pamoja na uimarishaji wa uwezo wa sekta na masuala mtambuka ikihusisha anuwai za jamii na mabadiliko ya tabianchi.
Ni vizuri kuelewa kuwa maji yanabaki kuwa uti wa mgongo wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Maji ni tegemeo kubwa kwa kufanikisha maendeleo katika sekta nyingine ambazo hutegemea upatikanaji wa maji kwa kiwango kikubwa; kuanzia afya, kilimo, nishati, usafirishaji hadi uzalishaji wa viwandani. Usimamizi bora wa rasilimali hii hauishii tu katika kuhakikisha upatikanaji wake, bali pia katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha maisha ya wananchi katika kazi za kila siku.
Kwa kulitambua hilo, Wizara ya Maji imeendelea kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maji kwa lengo la kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa wananchi wote. Malengo yaliyokuwa yamewekwa yalikuwa kufika asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini na asilimia 85 vijijini ifikapo Juni 2026. Tayari, mafanikio makubwa yalikuwa yamepatikana ambapo maeneo ya vijijini yalivuka lengo kwa kufika asilimia 85.2.
Hata hivyo, safari bado haijakamilika na inaendelea kuwafikia wananchi. Bado vipo vijiji 1,575 ambavyo havijafikiwa na huduma rasmi ya miundombinu ya huduma ya maji. Hali hiyo inaonyesha wazi kuwa ipo haja ya kuongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu ya maji, hasa katika maeneo ya pembezoni na yaliyo na uhaba wa upatikanaji wa vyanzo vya maji. Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi ili kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania atakayekosa kupata huduma hiyo muhimu.
Katika miji, juhudi zinaendelea kukamilisha miradi inayoendelea pamoja na kuanzisha miradi mipya ya kimkakati. Hii inajumuisha upanuzi wa mitandao ya usambazaji maji, ujenzi wa mitambo ya kutibu majitaka, ujenzi wa mabwawa na matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa rasilimali za maji na kupunguza kiwango cha upotevu wa maji (NRW).
Utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Tatu ulioanza Julai, 2022 unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2026.
Hata hivyo, kukamilika kwa hatua hiyo kunatarajiwa kuwa mwanzo wa safari mpya kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Katika mwelekeo huo, Sekta ya Maji imejipanga katika misingi mitatu mikuu: usalama wa maji, maji kwa maendeleo ya kiuchumi pamoja na uwekezaji endelevu katika sekta hiyo. Pamoja na hilo, Sekta Binafsi imefunguliwa miliango kufanikisha huduma ya maji kwa wananchi.
Ili kufanikisha maono hayo, sekta imejikita katika maeneo kadhaa ya kimkakati yanayojumuisha utekelezaji wa mpango kabambe wa kitaifa wa maji, utekelezaji wa gridi ya taifa ya maji pamoja na uendelezaji wa rasilimali za maji kupitia ujenzi wa mabwawa ya kimkakati na uendelezaji wa maji chini ya ardhi. Pia, kuwekwa mkazo katika kuboresha utoaji wa huduma, kujenga uwezo wa wataalamu wa sekta na kutafuta vyanzo mbadala vya fedha.
Vilevile, kama ilivyoelezwa ushirikishwaji wa sekta binafsi umepewa kipaumbele maalum, ukitambuliwa kama kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya maji.
Aidha, ujenzi wa miundombinu inayohimili athari za mabadiliko ya tabianchi umewekwa kama ajenda ya msingi, kutokana na changamoto zilizoongezeka za ukame, mafuriko na mabadiliko ya mifumo ya mvua.
Kaulimbiu ya “Maji na Jinsia” inaakisi umuhimu wa kipekee katika kufanikisha malengo hayo. Jamii, wakiwemo wanawake na watoto, ambao mara nyingi ndiyo wahusika wakuu katika upatikanaji na matumizi ya maji majumbani, wanapaswa kuwa sehemu ya maamuzi yanayohusu rasilimali hiyo. Kuwajengea uwezo na kuwapa nafasi sawa sio tu suala la haki, bali pia mkakati wa kuongeza ufanisi na uendelevu wa miradi ya maji.
Katika maeneo mengi ya vijijini, wanawake na watoto wanatumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji, hali inayowaathiri katika utunzaji wa familia, mahudhurio katika elimu na shughuli za kiuchumi. Kupatikana kwa maji karibu na makazi kutaleta mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza muda wa kupata elimu kwa watoto, kuboresha afya ya familia na kutoa fursa za kiuchumi kwa wanawake.
Kwa upande mwingine, ushiriki wa wanawake katika kamati za usimamizi wa maji wataendelea kuonesha mafanikio katika maeneo mengi. Wanawake wanaleta mtazamo wa kipekee katika usimamizi wa rasilimali, wakizingatia zaidi masuala ya usafi, matumizi bora ya maji, na uendelevu wa huduma.
Katika kufanikisha ajenda hiyo, ushirikiano kati ya Serikali na wadau mbalimbali umekuwa jambo lisiloepukika. Washirika wa maendeleo wamekuwa na mchango mkubwa katika kufadhili na kufanikisha miradi ya maji, kutoa utaalamu na kusaidia kujenga uwezo wa sekta ya maji. Mchango wao umeonekana wazi kupitia maboresho ya huduma za maji na usafi wa mazingira katika maeneo mengi ya nchi.
Ni dhahiri kuwa mafanikio yaliyopatikana yalikuwa matokeo ya ushirikishwaji na juhudi za pamoja. Hata hivyo, changamoto zilizopo zinahitaji mshikamano zaidi, ubunifu na dhamira ya dhati kutoka kwa kila mdau. Serikali imeonesha nia ya kuendelea kushirikiana na wadau wote ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
Kadri Tanzania inavyojimbanua kuelekea katika dira ya maendeleo ya muda mrefu, Sekta ya Maji inaendelea kubaki kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha ndoto hiyo.
Upatikanaji wa majisafi na salama sio tu haki ya msingi ya binadamu, bali pia chachu ya maendeleo ya taifa.
Mkutano wa Pamoja wa Mapitio ya Utekelezaji wa Programu ya Sekta ya Maji wa mwaka 2026 umekuwa hatua muhimu katika kuhakikisha kuwa sekta inaendelea kupiga hatua na kutekeleza malengo yake kwa ufanisi.
Aidha, umetoa fursa na kuwashirikisha wadau wote wa Sekta ya Maji kujifunza, kushirikiana na kuweka mkakati madhubuti kwa pamoja kwa siku zijazo; kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata huduma bora na endelevu ya majisafi na salama pamoja na usafi wa mazingira.


No comments:
Post a Comment