MRADI WA TACTIC KUONGEZA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WANANCHI KOROGWE MJI ‎ - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, April 27, 2026

MRADI WA TACTIC KUONGEZA FURSA ZA KIUCHUMI KWA WANANCHI KOROGWE MJI ‎



‎Na Mwandishi Wetu, Korogwe, Tanga

‎Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imeanza utekelezaji wa mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) unaolenga kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi katika Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga.

‎Hayo yameelezwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Bw. Burhan Ngulungu ambapo amesema kuwa takribani shilingi Bilioni 19 kupitia mradi wa TACTIC zitatumika katika ujenzi wa barabara za lami Km 10.4 na mifereji ya maji ya mvua itakayosaidia kuondoa maji katikati ya mji na kupeleka eneo la mto Pangani.

‎"Kuna barabara itaunganisha stendi ya Kijazi na soko la Kilole, hivyo barabara ikikamilika licha ya kupendezesha mji, wananchi pia wataweza kupata huduma za usafiri na usafishaji, mazingira bora ya kufanyia biashara kwa wajasiriamali na wafanyabiashara na pia kuongeza mapato ya halmashauri ya mji wa Korogwe", amesema.

‎Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Korogwe mjini CPA. Charles Njama amesema mradi huo unaotarajiwa kujenga barabara katika kata za Bagamoyo, Mgombezi, Mtonga, Manundu, Masuguru na Magunga unakwenda kuleta tabasamu la kudumu kwa wananchi wa Korogwe.

‎"Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mradi huu, barabara ya NMB-Magunga ni muhimu kwa wananchi wa Korogwe, Handeni, Lushoto na maeneo mengine kwasababu inapeleka wagonjwa hospitali ya Magunga, ikikamilika kwa kiwango cha lami itasaidia wagonjwa kufika hospitali bila usumbufu", amesema.

‎Naye, Mhandisi Charles Kamugisha Mratibu mradi wa TACTIC Korogwe Mji, ameeleza kuwa mradi unatarajiwa kukamilika tarehe 23 Januari, 2027 ambapo unahusisha ujenzi wa barabara ya NMB-Magunga Km 2.7, Bagamoyo-Mgombezi-Kibo Km 6.5, Kijazi Bus Stand-Kilole sokoni Km 1.2 pamoja na mifereji ya maji ya mvua Km 1.43 fedha za mkopo nafuu toka Benki ya Dunia.

‎Vilevile, Mhandisi Zakayo Magoro Meneja wa TARURA wilaya ya Korogwe amesema kuwa TARURA ina mtandao wa barabara za lami Km 16.1 kupitia mradi wa TACTIC zitaongezeka hadi kufikia Km 26.5 ambapo zikikamilika zitapendezesha mji, thamani ya ardhi itapanda na itapunguza gharama za matengenezo ya mara kwa mara.

‎Naye, Bw. Mohamed Dachi mkazi wa kata ya Mgombezi ambaye ni mkulima ameishukuru serikali kwa ujenzi wa barabara ya Bagamoyo hadi Kibo ambapo ikikamilika itaongeza fursa za kibiashara na kiuchumi kwani watasafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.

‎Bw. Salmin Sadala mkazi wa kata ya Manundu ambaye ni mfanyabiashara ndogondogo amesema kuwa baada ya kukamilika kwa mradi huo licha ya mji wa Korogwe kupendeza pia taa zikiwekwa watafanya biashara hadi usiku na kuchochea kukua kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi.








No comments:

Post a Comment