
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Programu ya “Sema na Waziri” imeendelea kuwa daraja muhimu kati ya serikali na wananchi, ambapo Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera amekuwa akisikiliza na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili Watanzania. Kupitia mawasiliano ya simu, wananchi wamepata fursa ya kueleza kero zao moja kwa moja na wameanza kupata majibu pamoja na hatua za awali za ufumbuzi.
Akizungumza Aprili 15,2026 baada ya kupokea simu na ujumbe kutoka kwa wananchi mbalimbali,Waziri Dkt.Homera amesema changamoto kubwa zilizojitokeza zimekuwa ni migogoro ya ardhi, masuala ya mirathi, ndoa za utotoni pamoja na ukatili wa kijinsia.
“Dhamira yetu kwa maelekezo ya Mhe. Rais Samia imekuwa ni kuona kwamba haki inatendeka kwa Watanzania wote, na sisi tumekuwa mstari wa mbele kuhakikisha masuala haya yote yamefanyiwa kazi,” amesema.
Ameongeza kuwa wizara yake imeendelea kushirikiana na wizara nyingine ili kuhakikisha changamoto hizo zimepatiwa ufumbuzi kwa wakati. “Tumekuwa na utaratibu wa kuwasiliana kati ya wizara, hivyo tumehakikisha kila changamoto imefika mahali sahihi na imeanza kushughulikiwa ipasavyo,” amesisitiza.
Katika siku hiyo, zaidi ya simu 20 na ujumbe zaidi ya 100 vimepokelewa, huku asilimia kubwa zikihusu migogoro ya ardhi na ukatili wa kijinsia. Waziri amebainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa kitengo hicho, jumla ya simu 2,236 zimepokelewa, ambapo asilimia 69 ya kesi zimefanyiwa kazi na asilimia 31 zimeendelea kushughulikiwa.
Miongoni mwa waliopiga simu ni Rahmu Mgema kutoka Mtwara, ambaye amelalamikia mgogoro wa ardhi unaohusisha eneo la uwanja wa ndege. “Wananchi takribani 350 tumedai eneo hilo ni letu, lakini hatujapata majibu ya kuridhisha hadi sasa,” amesema. Waziri ameahidi kulifuatilia suala hilo kwa kushirikiana na wizara husika na amewataka wananchi kuwa watulivu wakati suluhisho likiendelea kutafutwa.
Kisa kingine kimehusu Nasra kutoka Simiyu, ambaye ameripoti ukatili wa kijinsia dhidi ya mama yake. “Mama yangu amekuwa akipigwa na vitu vya ncha kali, kuna wakati alipigwa hadi kupasuka kichwa lakini ameogopa kutoa taarifa,” amesema kwa masikitiko. Waziri amempongeza kwa ujasiri wake na ameahidi kuwa hatua za haraka zimeanza kuchukuliwa kwa kushirikiana na mamlaka za eneo husika.
Kwa upande mwingine, mwananchi kutoka Mvomero amesimulia mateso aliyoyapitia baada ya kumsaidia mtoto wa miaka 11 kuepuka ndoa ya utotoni. “Nilimrudisha mtoto shule, lakini jamii imenigeuka na kunitishia maisha yangu hadi leo,” amesema. Waziri amemtia moyo na amemhakikishia kuwa serikali imeanza kuchukua hatua kuhakikisha usalama wake pamoja na haki ya mtoto inalindwa.
Waziri Dkt.Homera amesisitiza umuhimu wa wananchi kutoa taarifa mapema wanapokumbana na changamoto badala ya kuzificha. “Tumeendelea kutoa elimu kwamba wananchi wasikae kukumbatia changamoto, bali wazitoe ili zipatiwe ufumbuzi,” amesema.
Programu ya “Sema na Waziri” imeendelea kuendeshwa mara tatu kwa mwezi na imeendelea kuwapa wananchi nafasi ya kuwasilisha kero zao pamoja na kupata mrejesho wa yale yaliyowasilishwa awali, huku jitihada hizi zimeonesha dhamira ya serikali ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kuhakikisha haki imepatikana kwa wote bila ubaguzi.




No comments:
Post a Comment