
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akibofya kitufe ikiwa ni ishara ya kuzindua rasmi Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (wa pili kushoto), Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Khamis Ramadhan Abdalla (wa pili kulia), Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Juma Malik Akil (wa kwanza kulia), Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi. Rosemary Senyamule (kushoto) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel ( wa tatu kulia)

Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakionesha Vitabu vya Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 na Mkakati Wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 kwa Kipindi Cha Mwaka 2026–2036, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera hiyo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (Kulia), akipokea tuzo maalumu ya heshima kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoka kwa Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), kama Ishara ya kutambua mchango wake katika Mnyororo wa Ugavi, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (Kulia), akipokea tuzo maalumu ya Kutambua mchango wake katika kusimamia Mnyororo wa Ugavi, kutoka kwa Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati wa hafla ya uzinduzi wa Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025 Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), (Katikati Kulia), akiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), pamoja na viongozi wengine wakisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Ugavi Mwandamizi kutoka Idara ya Sera za Ununuzi wa Umma, Bi. Vaileth Mwakajisi (kushoto), kuhusu namna wanavyosimamia Mnyororo wa Ugavi, wakati wakitembelea mabanda ya maonesho katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma, alipofika kuzindua Sera Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025.

Meza Kuu ikiongozwa na Mgeni Rasmi Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Wizara ya Fedha, baada ya hafla ya uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
Na. Saidina Msangi na Joseph Mahumi, WF, Dodoma
Serikali imezindua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, inayolenga kufanya mageuzi makubwa katika mnyororo wa thamani, huku ikitajwa kuwa mwarobaini wa kudhibiti mianya ya upotevu wa rasilimali na kukuza ushiriki wa wazalishaji wa ndani katika uchumi wa Taifa.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akizindua Sera ya Taifa ya Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi ya Mwaka 2025, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa Sera hiyo, ambayo ni ya kwanza kuunganisha hatua zote za mnyororo wa ugavi kuanzia ununuzi hadi uondoshaji wa mali za umma, inalenga kuleta uwazi na ufanisi katika matumizi ya Serikali, ambapo zaidi ya asilimia 50 ya bajeti hupitia katika ununuzi wa bidhaa na huduma.
"Mnyororo wa ugavi umeimarishwa na kuwa chombo cha kimkakati cha kuongeza uzalishaji na ushindani wa Taifa letu katika masoko ya kikanda na kimataifa, hatua hiyo ya kisera inalenga kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Watanzania," alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa Sera hiyo mpya inaitambua rasmi Sekta Binafsi kama mdau wa kimkakati katika kuelekea Dira ya Maendeleo 2050, Serikali imepanga kuimarisha mazingira ya biashara ili kuruhusu uvumbuzi na ubunifu.
Aidha, alieleza kuwa makundi maalum yakiwemo ya wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu yamepewa kipaumbele kwa kuwekewa mazingira mahsusi yatakayowezesha ushiriki wao katika hatua mbalimbali za ugavi, jambo litakalosaidia kujenga uchumi jumuishi.
Mhe Dkt. Nchemba alifafanua kuwa katika kukabiliana na changamoto za urasimu na ubadhirifu, Serikali imesisitiza kuendelea kutumia mifumo ya kiteknolojia (TEHAMA) kama vile NeST, TANCIS, GIMIS na MUSE inayolenga kuimarisha uwazi na uwajibikaji kuanzia ngazi za chini hadi Taifa.
Mhe. Dkt. Nchemba alisisitiza Wadau wa Sekta Binafsi kuweka mikakati ya kuimarisha mifumo ya ushirikiano na sekta ya umma ili kunufaika kikamilifu na fursa zilizobainishwa katika Sera hiyo.
‘‘Mamlaka, Taasisi na Wadau wote waliopewa dhamana ya kusimamia utekelezaji wa Sera hii wabadilike na wahakikishe wanatekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na utawala wa sheria ili kufikia malengo na shabaha zilizoainishwa katika Sera hii’’, alisema Dkt. Nchemba.
Aliziagiza Mamlaka zote zinazohusika zihakikishe kuwa utekelezaji wa Sera hiyo unaimarisha ushiriki wa wazalishaji wa ndani, wafanyabiashara wadogo na wa kati, pamoja na makundi maalumu ya kijamii ili kufikia malengo jumuishi na usawa miongoni mwa washiriki.
Aidha, alizitaka Wizara na Taasisi zote za umma kufanya Mapitio ya Sera, Sheria, Kanuni na Miongozo mbalimbali inayokinzana na misingi ya Sera hiyo ili kuwa na mazingira rafiki katika usimamizi wa shughuli za Mnyororo wa Ugavi.
‘‘Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Taasisi na Mashirika ya Umma, Ofisi za Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Wadau wa Sekta Binafsi watekeleze Sera hii kwa Weledi, Uwazi na Uwajibikaji. Kufikiwa kwa malengo na shabaha za Sera hii yatategemea zaidi dhamira, fikra, mtizamo, uwazi, ushirikishwaji na uwajibikaji wa wadau wote katika ngazi zote za usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi,’’ alisisitiza Mhe. Dkt. Nchemba.
Aidha, alitoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Sera ili kuhakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa kama ilivyokusudiwa.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Fedha Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), alisema kuwa Sera hiyo inatoa mwongozo kuhusu shughuli zote za mnyororo wa ugavi- kuanzia hatua ya uandaaji wa mahitaji, ununuzi, ugomboaji, usafirishaji, upokeaji na urejeshaji, uhifadhi na utunzaji, matumizi na usambazaji, hadi uondoshaji wa mali katika sekta ya umma.
Alisema kuwa Sera hiyo haikuwa waraka wa kisera pekee, bali ni ahadi ya Serikali kwa wananchi; ahadi ya kusimamia rasilimali za Taifa kwa ufanisi, uwazi, uwajibikaji na tija, ili kila shilingi ya umma ilete thamani halisi kwa maendeleo ya Taifa letu.
Alifafanua kuwa Sera hiyo inalenga kuimarisha mfumo wa mnyororo wa ugavi katika sekta ya umma ili kurahisisha upatikanaji wa mahitaji ya Serikali kwa ubora unaostahili, kupata thamani halisi ya fedha, kurahisisha taratibu za ugomboaji na uondoshaji wa mizigo ya Serikali; kuimarisha mifumo ya upokeaji na urejeshaji wa mali, kuimarisha utunzaji, uhifadhi, matumizi na usambazaji wa bidhaa na mali za umma.
“Sera hii imelenga kuitambua sekta binafsi kwa ujumla kama nguzo ya kimkakati na kwa wadau wa ndani kama fursa ya kumiliki njia kuu za kiuchumi, kwa kuweka upendeleo maalumu katika baadhi ya maeneo;
Kuweka mazingira wezeshi kwa kampuni za ndani na makundi maalumu ya kijamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za mnyororo wa ugavi ili kuchochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi, kuongeza mnyororo wa thamani, kuzalisha ajira na kuongeza ushindani wa bidhaa na huduma za kitanzania katika soko la ndani, kikanda na kimataifa” alisisitiza Mhe. Balozi Omar.
Alisema kuwa jambo la muhimu zaidi, ni kuvutia uwekezaji katika sekta ya viwanda ili kuchochea mageuzi makubwa na ya haraka ya kiuchumi; na
Kupanua wigo wa mapato ya Serikali kwa kuimarisha misingi ya uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za mnyororo wa Ugavi,

No comments:
Post a Comment