SERIKALI YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA KUPITIA MRADI WA PAMOJA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, April 16, 2026

SERIKALI YAIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI WA KIJINSIA KUPITIA MRADI WA PAMOJA


Serikali imeendelea kuimarisha jitihada za kupambana na ukatili wa kijinsia kupitia utekelezaji wa Mradi wa PAMOJA, unaolenga kumaliza changamoto za ukatili dhidi ya wanawake pamoja na kuwawezesha kiuchumi na kuboresha ustawi wao katika jamii.

Akizungumza katika kikao cha kupitia na kuboresha rasimu ya mwongozo wa kushughulikia malalamiko yatakayojitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum Felister Mdemu amesema kuwa uwepo wa mwongozo huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki, uwazi na usawa vinazingatiwa kwa wanufaika wote.

Ameeleza kuwa mradi wa PAMOJA hauishii katika kuwawezesha wanawake kiuchumi pekee, bali pia unalenga kuzuia na kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoathiri maendeleo ya wanawake na jamii kwa ujumla.
L
Katika kufanikisha hilo, amesema mradi umeweka mkazo katika ujenzi wa vituo vya kulelea watoto, hatua itakayowawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali bila kukwamishwa na majukumu ya ulezi.

Kwa upande wake Juliana Kibonde Mkurugenzi Msaidizi mradi huo amesema uwekezaji unaofanyika ni chachu ya kuimarisha ustawi wa wanawake na familia kwa ujumla, sambamba na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ameongeza kuwa huduma zitakazotolewa kupitia vituo hivyo zitaunganishwa katika mifumo ya kidijitali ili kuongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Naye Mratibu wa Mradi wa PAMOJA, Adventina Kato amesema mradi huo umelenga kupunguza kwa kiwango kikubwa, na hatimaye kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake, ambavyo vimekuwa tishio katika jamii. Amebainisha kuwa kuwawezesha wanawake kiuchumi ni njia mojawapo ya kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kujilinda dhidi ya mazingira hatarishi.

Kwa upande wake, Afisa Sheria Mkuu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Happy Msimbe amesema mwongozo huo unatarajiwa kuleta matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kupunguza malalamiko, kuimarisha usimamizi wa haki na kuongeza imani ya wananchi katika utekelezaji wa mradi huo.

Mradi wa PAMOJA unatarajiwa kuwa suluhisho endelevu katika kupambana na ukatili wa kijinsia huku ukichangia maendeleo jumuishi kwa wanawake na jamii kwa ujumla.



No comments:

Post a Comment