
Na OWM (KAM), Njombe
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amewataka waajili nchini kutekeleza Amri ya nyongeza ya Kima cha Chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi kama inavyofanywa na Serikali.
Nyamhokya ametoa kauli hiyo leo Aprili 27, 2026 alipotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano katika maonesho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayoendelea mkoani Njombe.
Alisema Serikali ilitangaza kima hicho cha chini cha mishahara ambacho kimeanza kutumika mwezi Januari mwaka huu, ambapo hadi sasa takwimu zinaonesha ni takribani asilimia 80 tu ya waajili katika sekta binafsi wameanza kutekeleza.
“Nitoe wito kwa waajili wa sekta binafsi nchini kutekeleza amri hii ya serikali kwa kuongeza mishahara husika... hatua itakayochangia ustawi na morali ya wafanyakazi,” alisisitiza Rais huyo wa TUCTA.
Akiwa katika banda hilo, Nyamhokya alipokea maelezo ya elimu zinazotolewa, ikiwemo elimu ya huduma za ajira, kinga ya jamii, sheria za kazi nchini pamoja na mahusiano baina ya Serikali na Makundi ya Kijamii yanayo jumuisha Taasisi za Dini, Mashirika yasiyo ya Kiserikali,Wadau wa Siasa na Asasi za kiraia.
Alipongeza maafisa wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa elimu wanayoitoa kwa umma kwenye maonesho hayo, akisema inaakisi huduma za wizara kwa wananchi na wafanyakazi.
Pia, Nyamhokya amewaasa wananchi na wafanyakazi kuendelea kutembelea banda hilo ili kupata elimu zaidi ikiwemo elimu ya kinga ya jamii.
Katika hatua nyingine, Rais wa TUCTA amewasihi wafanyakazi mkoani Njombe na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika sherehe za Mei Mosi zinazotarajiwa kufanyika kitaifa katika mkoa huo.

No comments:
Post a Comment