
Na Atley Kuni, WAF-Morogoro
Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha afya ya jamii na kukabiliana na milipuko ya ugonjwa wa kuambukiza wa kipindupindu kwa kuendesha mafunzo maalum yanayolenga kuongeza utayari na uwezo wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa ngazi ya msingi.
Akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wataalam wa Maabara nchini April 27, 2026 mkoani Morogoro, Bw. Seif Abdul kwa niaba ya Mkurugenzi wa Maabara ya taifa amesema mafunzo hayo, yanahusisha wilaya za mikoa iliyobainika kuwa katika hatari juu ya mlipuko wa kipindupindu.
"Mikoa ya Songwe, Rukwa, Mbeya, Iringa, Morogoro, Singida, Dodoma, Manyara, Tanga, Arusha, Mara, Kigoma, Mwanza, Dar es Salaam na Ruvuma ni miongoni mwa mikoa ambayo imekuwa kwenye hatari kubwa ya maambukizi" amesema Abdul.
Abdul amesema kuwa, lengo kuu la mafunzo hayo ni kuimarisha utayari wa wataalam kwa ngazi za mikoa na wilaya ili wawe na utayari wa mwitikio wa haraka na wenye ufanisi na tija wakati mlipuko wa kipindupindu unapotokea.
Akitoa neno la utangulizi Mmoja ya wakufunzi kutoka Maabara ya Taifa Bw. Emmanul Magembe amesema, washiriki wakati wa mafunzo watapatiwa uelewa kuhusu miongozo ya kimataifa ya ufuatiliaji wa kipindupindu pamoja na matumizi ya programu maalum ya simu (cholera app) wakati wa kukabiliana na milipuko.
Katika hatua nyingine, mafunzo hayo pia yanalenga kujenga uwezo wa wataalamu wa afya katika ukusanyaji sahihi wa sampuli za ugonjwa huo na usafirishaji wake kwa ajili ya uchunguzi katika maabara ya taifa.
"Tunategemea washiriki watapata fursa ya kubadilishana uzoefu.
Kwa mujibu wa waandaaji, matokeo yanayotarajiwa kutokana na mafunzo hayo ni pamoja na kila kituo cha afya kuwa na uwezo wa kufanya ukusanyaji na usafirishaji sahihi wa sampuli, kutoa majibu ya haraka kwa kutumia vipimo vya uchunguzi wa haraka (RDT), pamoja na kutumia ipasavyo programu ya GTFCC wakati wa milipuko.
Naye Mratibu wa mradi wa KOFI Olimpia Machange, ambao wanashirikiana na Serikali kutoa mafunzo hayo, amesema mradi huo wa miaka mitano ulianza kuwapatia mafunzo wataalam ngazi ya Mikoa na sasa wameshuka ngazi ya Wilaya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mifumo ya afya inaimarika hapa Nchini na kuwa tayari wakati wote.








No comments:
Post a Comment