
Mwenyekiti wa Tume ya kuchunguza vurugu za uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Jaji Othman Chande, amesema tume hiyo iko huru na haiikingiliwa na mamlaka yoyote, akikanusha madai kuwa muda wa kazi yake umeongezwa ili kuruhusu kuhaririwa kwa ripoti yake.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam leo, Jaji Chande alisema kuwa tume hiyo ina mamlaka kamili ya mwisho juu ya ripoti yake na haitoi nafasi kwa mtu yeyote kuingilia kazi yake.
"Tume inajitegemea kwa kila kitu. Tume yenyewe ndiyo mhariri, na mamlaka iliyotupa jukumu tutakutana nayo wakati wa kukabidhi ripoti ya mwisho, hatuna mtu yoyote katikati, hatuna dalali," alisisitiza.
Kumekuwa na madai kutoka kwa baadhi ya wadau hasa wanaharakati mitandaoni nchini Tanzania wanaoona kwamba kuongezwa kwa muda wa tume hiyo mara mbili kunalenga kutoa nafasi kwa mamlaka fulani 'kuchakachua' yaliyomo kwenye ripoti hiyo.
Hata hivyo, Jaji Chande alieleza kuwa sababu kuu ya kuongeza muda ni kupanuka kwa wigo wa kazi pamoja na ongezeko la ushahidi unaokusanywa"
Aliongeza kuwa tume imepokea ushahidi mwingi kutoka kwa wananchi na wadau mbalimbali, pamoja na ushauri wa kitaalamu ambao unahitaji kuchambuliwa kwa kina kabla ya kukamilisha ripoti.
"Tunachambua ushahidi kwa kina ili kuhakikisha ripoti yetu inakuwa na ubora unaotakiwa, na pia itatolewa kwa lugha ya Kiswahili na tafsiri ya Kiingereza," alifafanua.

No comments:
Post a Comment