Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ameonesha kuridhishwa kwake na kazi kubwa iliyofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), akiupongeza kwa usimamizi thabiti wa miradi 81 ya dharura iliyotekelezwa kote nchini.
Miradi hiyo, iliyohusisha ujenzi wa madaraja na makalvati kupitia mpango maalum wa CERC, imeelezwa kuwa mfano wa mafanikio ya kitaifa katika kukabiliana na changamoto za miundombinu hususan nyakati za mvua na mafuriko.
Akizungumza mkoani Morogoro wakati akifungua Mkutano wa 21 wa Baraza la Wafanyakazi wa TANROADS, Ulega amesisitiza kuwa miradi hiyo si tu imekamilika kwa wakati, bali pia imejengwa kwa viwango vya juu vya ubora na Makandarasi wazawa jambo linaloonesha kukua kwa uwezo wa ndani wa kitaalamu.
Waziri Ulega amemshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia upatikanaji wa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo, akibainisha kuwa uwekezaji huo umeanza kuzaa matunda.
Ameongeza kuwa licha ya mvua zinazoendelea kunyesha nchini mwaka huu, athari zake zimepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma hali inayochangiwa na ubora wa miundombinu iliyojengwa.
“Miradi hii ya dharura ni alama ya uwezo wa wataalam wetu wa TANROADS katika kusimamia na kutekeleza kazi kwa umahiri mkubwa. Ni mfano hai wa namna tunavyoweza kukabiliana na changamoto za mafuriko nchini”, amesisitiza Ulega, huku akihimiza kuendelea kufanyika tathmini ya kina ili kubaini maeneo mengine yanayohitaji madaraja ya kisasa kama hayo.
Katika kuimarisha utendaji wa Taasisi hiyo, Waziri Ulega amewataka viongozi na watumishi wa TANROADS kote nchini kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na ubunifu, sambamba na kuzingatia nidhamu kazini.
Amesisitiza umuhimu wa kulinda na kuendeleza misingi iliyoasisiwa na waanzilishi wa Wakala huo kwa lengo la kuijenga Tanzania yenye miundombinu imara.
Aidha, ametoa maelekezo mahsusi ya kuhakikisha matengenezo ya barabara na madaraja yanafanyika kwa wakati ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.
Pia, ameelekeza utekelezaji wa mpango wa kupendezesha barabara kwa kupanda miti ya kivuli na matunda takribani 1,000 kwa kila mkoa, pamoja na kuimarisha uwekaji wa taa za barabarani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mussa Kilakala ameishukuru Serikali kupita Wizara ya Ujenzi kwa kutoa malipo ya awali Mkandarasi anayejenga barabara ya Bigwa - Kisaki (km 78) kwa kiwango cha lami na kueleza kuwa mradi huo tayari umeanza huku akifafanua kuwa wananchi wa Kinole na Mbingu watakuwa wanufaika wakubwa wa ujenzi wa miundombinu hiyo.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, ameeleza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu unalenga kuimarisha ushirikishwaji wa wafanyakazi katika maamuzi ya kiutendaji na kupanga mikakati ya maendeleo ya Taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, akimwakilisha Katibu Mkuu, Bw. Karim Mkorehe amemhakikishia Waziri Ulega kuwa TANROADS itaendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa Taasisi na kuhakikisha wananchi wanapata miundombinu bora, salama na ya kisasa.









No comments:
Post a Comment