USALAMA NA USTAWI WA MFANYAKAZI SI CHAGUO, NI KIPAUMBELE CHETU - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 29, 2026

USALAMA NA USTAWI WA MFANYAKAZI SI CHAGUO, NI KIPAUMBELE CHETU


Kampuni ya GASCO imeeleza kuwa usalama na ustawi wa mfanyakazi ni nguzo muhimu katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuhakikisha mazingira salama, rafiki na yenye kuchochea tija kazini.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Mazingira Mwandamizi wa GASCO, Bi. Suzana Masaba, wakati wa maonesho ya maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani (OSHA) yanayofanyika kitaifa mkoani Njombe.

Masaba alisema kampuni hiyo imeweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa salama na wenye afya njema wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa mfanyakazi salama ni msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote.

“Usalama na ustawi wa mfanyakazi si chaguo, ni kipaumbele chetu. Tunaamini mfanyakazi salama na mwenye afya njema ndiye msingi wa mafanikio ya taasisi yoyote,” alisema Masaba.

Amefafanua kuwa kupitia ushiriki wake katika maonesho hayo, GASCO imeonyesha kwa vitendo utekelezaji wa sera na mikakati yake ya usalama kazini, ikiwemo matumizi ya vifaa vya kisasa vya kujikinga (PPE) vinavyosaidia wafanyakazi kujilinda wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.

Aidha, alisema kampuni hiyo imeendelea kuwekeza katika mafunzo ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wake ili kuwajengea uelewa mpana kuhusu masuala ya usalama na afya kazini, pamoja na namna ya kukabiliana na hatari zinazoweza kujitokeza katika mazingira ya kazi.

Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi, kupunguza ajali kazini na kuimarisha utamaduni wa kujali maisha ya kila mfanyakazi.

Masaba alibainisha pia kuwa shughuli za GASCO zinaendana na kauli mbiu ya maonesho ya OSHA ya mwaka huu isemayo, “Mazingira bora ya kisaikolojia na kijamii kazini ni njia ya kuimarisha ustawi wa wafanyakazi na kujenga taasisi imara.”

Kwa mujibu wake, ushiriki wa GASCO katika maonesho hayo ni uthibitisho wa dhamira ya kampuni hiyo kuhakikisha wafanyakazi wake wanakuwa salama, wenye afya njema na wenye motisha ya kuchangia maendeleo ya sekta ya gesi na taifa kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment