VIONGOZI WA WACHIMBAJI WASHAURIWA KUWEKA UZALENDO KULINDA RASILIMALI MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, April 25, 2026

VIONGOZI WA WACHIMBAJI WASHAURIWA KUWEKA UZALENDO KULINDA RASILIMALI MADINI


Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Viongozi wa Wachimbaji Wadogo wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) wametakiwa kutanguliza Uzalendo na Uadilifu katika kusimamia rasilimali madini ili utajiri huo uendelee kuwanufaisha Watanzania wa leo na vizazi vijavyo.

Rai hiyo imetolewa leo Aprili 25, 2026 na Kamishna wa Madini Dkt. AbdulrahMan Mwanga wakati akiwasilisha mada maalum ya kuwajengea uwezo viongozi wa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini yaliyofanyika Dodoma.

Dkt. Mwanga amesema kuwa, rasilimali madini ni nguzo kwa uchumi wa taifa ambayo inatoa fursa za kiuchumi kwa watanzania kunufaika moja kwa moja kupitia mapato au miradi mikubwa ya kitaifa inayotokana na sekta ya madini kupitia programu maalum ya CSR na Local Content.

Dkt. Mwanga ameongeza kuwa, uchimbaji madini unaendana na utunzaji wa mazingira jambo la kikakati kwa taifa na ustawi wa jamii nzima lengo ni kutekeleza takwa la kisheria linalohusu Usalama Mahali Pa Kazi.

Kuhusu utoroshaji wa madini, Dkt. Mwanga amefafanua kuwa, suala la utoroshaji wa madini ni kinyume na Sheria ya Madini Sura Namba 123 na Sheria nyingine za nchi, hivyo amewaasa viongozi hao kutojihusisha na mifumo yoyote ya utoroshaji madini nchini.

Aidha, ameongeza kuwa , utoroshaji madini unasababisha hasara kubwa za kiuchumi na kijamii hii ni kutokana na Serikali kukosa mapato ya kodi jambo linalopelekea kurudisha nyuma maendeleo ya taifa.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Madini Augustino Olal amesema, mafunzo hayo ya kimkakati yameletwa kwa mpango maalum ambao utaleta matokeo chanya kwenye uongozi katika sehemu za kazi na kuongeza uzalishaji madini nchini.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt.Venance Mwase amesema lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uwezo viongozi wote wanaosimamia kamati mbalimbali ndani ya FEMATA ili wapate maarifa mbalimbali ya kufanya maamuzi na kujenga ushirikiano mzuri kulingana na mada zitakazotolewa.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Wachimbaji Wadogo Tanzania ( FEMATA) John Bina ameiomba STAMICO kutoa mafunzo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa kupewa semina kuhusu Sheria za Madini na Kanuni zake ili kuondoa mgongano wa maslahi katika mnyororo mzima wa thamani madini.

Mwenyekiti wa Chama cha Wazalishaji Chumvi Tanzania (TAPSA) Bi.Hawa Ghasia , ameipongeza Wizara ya Madini kupitia STAMICO kwa kutatua changamoto 7 kati ya 13 ambapo nyingine zilizobaki zikiendelea kutafutiwa uvumbuzi.

Ghasia ameishukuru Serikali kwa kuweka miundombinu mizuri kwenye mashamba ya chumvi pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata chumvi kilichombioni kukamilika.

Pamoja na mambo mengine , vyama vingine kikiwemo chama cha CHAWATA, TAWOMA, vimeipongeza Wizara ya Madini kwa ushirikiano mzuri unaoendelea katika sekta ya madini.

No comments:

Post a Comment