WANACHUO UDOM WAPEWA ELIMU YA SHERIA, WATAKIWA KUENEZA UFAHAMU KWA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, April 28, 2026

WANACHUO UDOM WAPEWA ELIMU YA SHERIA, WATAKIWA KUENEZA UFAHAMU KWA JAMII


Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wizara ya Katiba na Sheria imesema matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni nyenzo muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma za msaada wa sheria, huku yakitajwa kuwa daraja la kuwafikia wananchi wengi kwa wakati.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Huduma za Msaada wa Sheria, Esther Msambazi, alipokutana na wanachuo wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) katika mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya Mama Samia Legal Aid awamu ya pili.

Msambazi amesema lengo la mdahalo huo ni kuwajengea uwezo wanachuo hao kuelewa masuala ya kisheria, kutambua haki zao, pamoja na kufahamu wapi pa kupata huduma za msaada wa sheria wanapokumbana na changamoto.


“Tunataka vijana wawe na uelewa wa kutosha wa sheria ili waweze kujisaidia wao wenyewe, lakini pia wawe mabalozi wa elimu ya kisheria kwa jamii inayowazunguka,” amesema Msambazi.

Ameeleza kuwa Wizara ya Katiba na Sheria ina jukumu la kuratibu na kusimamia upatikanaji wa haki nchini, hivyo inaendelea kutumia mbinu mbalimbali ikiwemo TEHAMA ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Katika mdahalo huo, wanachuo walielimishwa kuhusu ukatili wa kijinsia, matumizi chanya ya mitandao ya kijamii pamoja na athari za matumizi mabaya ya teknolojia.

Aidha, Msambazi amesisitiza kuwa matumizi sahihi ya TEHAMA yanaweza kuwasaidia vijana kupata taarifa sahihi za kisheria kwa urahisi, kuwasiliana na watoa huduma za msaada wa sheria, na hivyo kupunguza changamoto za upatikanaji wa haki.


Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Mahakama ya Tanzania, Bw. Kalege Enock, aliipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuwashirikisha vijana katika mdahalo huo wenye mada ya “Ushiriki wa vijana katika utoaji wa huduma za kisheria.”

Amesema ushiriki wa vijana ni muhimu katika kujenga jamii yenye utulivu na amani, akibainisha kuwa kampeni ya Mama Samia Legal Aid awamu ya pili ina matarajio makubwa ya kuleta matokeo chanya.

Kuhusu utatuzi wa migogoro, Enock ameeleza umuhimu wa kutumia njia mbadala nje ya Mahakama, akisema mifumo ya kimila na kifamilia inaweza kusaidia kupunguza mzigo wa kesi mahakamani.

“Njia mbadala za utatuzi wa migogoro zina faida kubwa kwani hazihusishi taratibu ndefu za kisheria, zinatoa nafasi kwa wahusika kuzungumza kwa uhuru, na husaidia kumaliza migogoro bila kuibua mingine,” amesema.


Naye Amidi wa Shule Kuu ya Sheria Chuo Kikuu cha Dodoma, Dkt. Elia Mwanga, amesema mdahalo huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuwajengea uelewa vijana kuhusu masuala ya msaada wa kisheria.

Amesisitiza kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa na wanapaswa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa msaada wa kisheria pamoja na kuchangia maendeleo ya nchi.
“Kwa kuwa chuo hiki kina wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, watakuwa mabalozi wazuri wa kusambaza elimu ya kisheria na kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo kwa urahisi,” amesema Dkt. Mwanga.

Nao baadhi ya wanachuo walioshiriki mdahalo huo walisema wamepata uelewa mpana wa masuala ya sheria, ikiwemo namna ya kutambua na kutetea haki zao bila kukiuka Katiba ya nchi.

Kwa ujumla, mdahalo huo umeonesha mwamko mkubwa wa vijana kushiriki katika masuala ya kisheria na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha haki inapatikana kwa wananchi wote.

No comments:

Post a Comment