BARA LA AFRIKA LIWEKE MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA VITA MASHARIKI YA KATI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 3, 2026

BARA LA AFRIKA LIWEKE MIKAKATI YA KUKABILIANA NA ATHARI ZA VITA MASHARIKI YA KATI

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akishiriki Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi na Magavana wa Benki Kuu wa Afrika wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Uchumi Afrika (UNECA), unaofanyika jijini Tangier nchini Morocco.
ambao pamoja na mambo mengine unajadili athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati namna ulivyoleta athari hasi za kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika na namna ya kukabiliana nazo. Mkutano huo umewashirikisha pia Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji Mhe. Dkt. Pius Chaya na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha, Tangier, Morocco)


Na Benny Mwaipaja, Tangier-Morocco


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuwa na mtazamo wa pamoja katika kubuni na kutekeleza mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu, ambayo ni endelevu na jumuishi, itakayopunguza utegemezi na kuimarisha
uthabiti wa uchumi wa Bara la Afrika ili kukabiliana na majanga na migogoro ya vita inayoendelea duniani.

Mhe. Balozi Omar alitoa wito huo jijini Tangier nchini Morocco, katika Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Fedha, Mipango na Maendeleo ya Uchumi na Magavana wa Benki Kuu wa Afrika, wakati akichangia mjadala kufuatia taarifa ya Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia Uchumi Afrika (UNECA), inayochambua athari za mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati namna ulivyoleta athari hasi za kiuchumi na kijamii katika Bara la Afrika.

Alibainisha kuwa baadhi ya nchi za Afrika, hususan zile zinazotegemea sekta ya utalii, zinaweza kuathirika zaidi na Mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati.

Kwa upande wa Tanzania, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mgogoro huo kupitia ushirikiano katika Wizara za Kisekta na Taasisi zake, ili kubaini hatua stahiki za kisera zitakazolinda ustawi wa uchumi na maslahi ya wananchi.

Vilivile, alieleza kuwa pamoja na kwamba mgogoro huo umeathiri mtiririko wa biashara kwa kuwa ukanda wa Mashariki ya Kati ni lango muhimu la biashara kati ya Afrika na masoko ya kimataifa. Hivyo, ni muda muafaka wa Afrika kuona umuhimu wa kuwa na njia mbadala ya kufanya biashara hususan miongoni mwa nchi wanachama.

Mheshimiwa Balozi Omar alisisitiza kuwa kwa muda mrefu Afrika imekuwa ikijadili umuhimu wa kutumia rasilimali zake ipasavyo, na kwamba hali ya sasa inatoa fursa ya kuchukua hatua madhubuti za kujitegemea kwa kutumia rasilimali zake.

Alifafanua kuwa Bara la Afrika lina rasilimali za kutosha, ikiwemo mafuta na mbolea, ambazo zinaweza kuzalishwa na kupatikana ndani ya Bara kupitia ushirikiano, hususan Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Mhe. Balozi Omar alieleza kuhusu umuhimu wa kuendelea na majadiliano chini ya uratibu wa UNECA kuhusu mageuzi katika mifumo inayosimamia maamuzi na sera za kifedha duniani (Global Financial Architecture), ili Afrika iweze kuwa na sauti moja yenye nguvu katika upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa gharama nafuu kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Alisisitiza kuwa mafanikio ya mageuzi hayo yatategemea mshikamano na ushirikiano thabiti wa nchi za Afrika.

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo, walieleza kuwa ili kukabiliana na mizozo hiyo nchi za Afrika zinahitaji kuweka sera na mikakati ya kuondoa vikwazo vya ufanyaji biashara na upitishaji wa bidhaa kwa kufungua mipaka yake.

Aidha, walishauri kuwa umefika wakati wa nchi za Afrika kuzalisha mafuta yake na kutumia vyanzo vingine mbadala vya nishati ili kukabiliana na uhaba wa mafuta na kupanda kwa bidhaa hiyo muhimu katika uzalishaji na uchumi wa mataifa hayo.

No comments:

Post a Comment