TAIFA GESI YAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI HANDENI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 3, 2026

TAIFA GESI YAHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI HANDENI







Na Oscar Assenga

Kampuni ya Taifa Gesi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuunga mkono sera ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.

Akizungumza katika tamasha lililofanyika wilayani Handeni, Mkurugenzi wa Masoko wa Taifa Gesi, Oscar Shelukindo, alisema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika matamasha ya kijamii tangu mwaka jana kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya gesi safi.

Alisema kuwa katika tamasha hilo, wameelekeza nguvu zaidi kwa wakazi wa Handeni, hususan Kata ya Mdoe, ili kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuwapa uelewa sahihi kuhusu faida za kutumia nishati hiyo.

“Tunafurahi kuwa hapa leo kutoa elimu ya matumizi ya gesi safi, kuondoa hofu kwa wananchi na kuwahamasisha kuachana na matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira. Pia tunatoa gesi kwa bei nafuu ili kuwavutia zaidi kuitumia,” alisema Shelukindo.

Alifafanua kuwa bado kuna wananchi wengi ambao wana hofu au uelewa mdogo kuhusu matumizi ya gesi ya kupikia, hali inayowafanya kuendelea kutumia nishati kama kuni na mkaa, ambazo si rafiki kwa mazingira na pia zina madhara kiafya.


Kwa mujibu wa Shelukindo, utoaji wa elimu hiyo unalenga kubadili mtazamo wa jamii na kuwasaidia wananchi kuelewa kuwa gesi ni salama, nafuu kwa muda mrefu na rahisi kutumia.

Aidha, alisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mchango wa sekta binafsi katika kusaidia juhudi za Serikali za kulinda mazingira, kupunguza ukataji wa miti na kuboresha afya za wananchi kupitia matumizi ya nishati safi.

Wananchi waliohudhuria tamasha hilo walipata fursa ya kuuliza maswali, kujifunza matumizi sahihi ya gesi pamoja na kununua bidhaa za gesi kwa bei iliyopunguzwa.

Kwa ujumla, jitihada za Taifa Gesi zinaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, hatua inayotarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika jamii, hususan maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment