
Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe ameilekeza TARURA na Manispaa ya Kinondoni kuhakikisha ujenzi wa barabara ya Togo unakamilika mwezi Juni, 2026 na mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kimario (Brazil) unasainiwa Mei 25, 2026, ili kuwaondolea adha wananchi wa Kinondoni na watumiaji wengine wa barabara hizo zinazojengwa kwa kiwango cha lami kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Jiji la Dar es Salaam Awamu ya Pili (DMDP II).
Prof. Shemdoe ametoa maelekezo hayo leo Mei 10, 2026 Kinondoni Jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na ofisi yake kupitia Wakala ya Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), aliyoifanya kutokana na ombi la wananchi wa Kinondoni kupitia kwa Mbunge wao Mhe. Abbas Tarimba.
“Tunaondoka hapa tukikubaliana kwamba barabara ya Togo itakamilika Juni 2026 na mkataba wa ujenzi wa barabara ya Kimario (Brazil) utasainiwa Mei 25, 2026 hivyo waheshimiwa Madiwani mfuatilie utekelezaji wa maelekezo haya,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amemtaka Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam Mhandisi Geofrey Mkinga na Meneja wa TARURA Wilaya ya Kinondoni Mhandisi Edwin Kabwote kuhakikisha wanasimamia barabara hizo zikamilike kwa wakati ili kuwaondolea adha wananchi wa Kinondoni na watumiaji wote wa barabara hizo hususani kipindi hiki cha mvua.
Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ujenzi wa barabara 17 za DMDP II katika wilaya ya Kinondoni zilizogharimu Shilingi Bilioni 97.7 ambazo zina jumla ya urefu wa wa kilometa 36.483.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Kinondoni Mhe. Abbas Tarimba amemshukuru Waziri wa TAMISEMI Prof. Riziki Shemdoe kwa kufanya ziara ya kukagua miradi hiyo ya maendeleo na kutoa maelekezo mahususi ya kuikamilisha, na kuongeza kuwa wananchi wamejionea wenyewe usikivu wa Waziri huyo wa Serikali ya Awamu ya Sita ambaye ametembelea miradi ya maendeleo jimboni kwake ikiwa ni siku ya jumapili ambayo anapaswa kupumzika.





No comments:
Post a Comment