BIMA YA AFYA YAPEWA KIPAUMBELE NA WADAU, PROF. SHEMDOE AWATAKA WATANZANIA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 8, 2026

BIMA YA AFYA YAPEWA KIPAUMBELE NA WADAU, PROF. SHEMDOE AWATAKA WATANZANIA KUJIUNGA NA BIMA YA AFYA


Na OWM - TAMISEMI, Dar es Salaam


Mkutano wa 25 wa mwaka wa pamoja wa Sera ya Sekta ya Afya umepitia na kuthibitisha vipaumbele vya Sekta ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/27 ikiwepo utekelezaji wa bima ya afya kwa wote, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Prof. Riziki Shemdoe akitoa wito kwa watanzania kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Rais ya kuwawezesha wananchi kumudu gharama za matibabu.

Prof. Shemdoe ametoa wito huo leo Mei 08, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Mkutano wa Sera wa kupitia na kuthibitisha vipaumbele vya Sekta ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/27 katika Hoteli ya Protea, ambao awali ulifunguliwa na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa.

“Bima ya afya kwa wote imejadiliwa na kusainiwa na wadau ikiwa ni moja ya kipaumbele cha sekta ya afya kwa mwaka 2026/27, hivyo ninawaomba watanzania wote tujiunge na bima ya afya ambayo ni muhimu katika ulinzi wa afya zetu,” amesistiza Prof. Shemdoe.

Aidha, Prof. Shemdoe amewataka watanzania wenye uwezo wa kiuchumi kuwawezesha wengine ambao hawana uwezo wa kujiunga Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote ili watanzania wote wanufaike na uwepo wa huduma ya bima ya afya kwa wote.


Kwa upande wake, Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema kuwa wizara yake imekutana na wadau wa sekta ya Afya ili kujadili kwa pamoja changamoto na mafanikio yaliyopatikana katika mwaka wa fedha 2025/26, ikiwa ni pamoja na kupitia na kuthibitisha vipaumbele vitakavyotekelezwa na Sekta ya Afya kwa Mwaka wa Fedha 2026/27.

“Leo baada ya kujadiliana na wadau wote wa sekta ya afya, tumesaini makubaliano ya vipaumbele ambavyo kwa pamoja tutavitekeleza katika mwaka wa fedha 2026/27 ili kulinda afya za watanzania wote,” amesema Mhe. Mchengerwa.

No comments:

Post a Comment