DKT. MWIGULU AAGIZA ITAFUTWE SULUHU YA KUDUMU DARAJA LA MAGOLE–DUMILA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 8, 2026

DKT. MWIGULU AAGIZA ITAFUTWE SULUHU YA KUDUMU DARAJA LA MAGOLE–DUMILA



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akikagua ujenzi wa Daraja la Magole–Dumila katika Mto Mkundi Dumila mkoani Morogoro leo tarehe 8 Mei, 2026. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi wa Dumila mkoani Morogoro waliojitokeza wakati alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Magole-Dumila mkoani Morogoro leo tarehe 8 Mei, 2026. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU



Muonekano wa Daraja la Magole-Dumila mkoani Morogoro ambalo leo tarehe 8 Mei, 2026 Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nnchemba alifanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wake. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mkutano wa hadhara alioufanya katika eneo la Magoweko, Gairo mkoani Morogoro leo tarehe 8 Mei, 2026. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi waliojitokeza katika hafla ya uzinduzi wa hoteli ya Mikumi Wildlife katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, wilayani Kilosa, mkoani Morogoro leo tarehe 8 Mei, 2026. PICHA NA OFISI YA WAZIRI MKUU


Na Mwandishi Wetu, Morogoro 


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amefanya ukaguzi wa daraja la Magole lililopo Dumila katika Mto Mkundi wilayani Kilosa na kuagiza uongozi wa TANROADS utafute suluhu ya kudumu ya changamoto inayolikabili daraja hilo ya kujaa maji na mchanga kila mwaka.


Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Mei 8, 2026) wakati akizungumza na wananchi waliofika darajani hapo kumsikiliza na akamtaka Meneja wa TANROADS Mkoa wa Morogoro ashirikiane na wataalamu wengine kuandaa utaratibu wa kuwaruhusu wananchi kuchimba mchanga katika eneo hilo kwa kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, ili kusaidia kupunguza mzigo wa gharama za Serikali na wakati huohuo kulinda miundombinu ya daraja hilo.


“Meneja wa TANROADS na wenzako wote ratibuni eneo ambalo tunahangaika kutoa mchanga na hatuna bajeti, wananchi muwaruhusu watoe mchanga huo kwa utaratibu wa kitaalamu,” amesisitiza Waziri Mkuu.


Akitoa taarifa kuhusu hali ya eneo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima amesema kuwa kwa muda mrefu daraja hilo limekuwa likikumbwa na changamoto ya kurundikana kwa mchanga unaosababishwa na mtiririko mkubwa wa maji katika mto huo, hali inayohatarisha usalama, ustawi na uimara wa daraja hilo.


Ameeleza kuwa daraja hilo ni la kimkakati linalounganisha Wilaya za Kilosa na Gairo mkoani Morogoro, sambamba na kuwa sehemu ya njia kuu ya usafirishaji wa magari kutoka Dar es Salaam kupitia Morogoro kuelekea Dodoma na mikoa mingine ya nchi.


Kwa mujibu wa Meneja wa TANROADS wa Mkoa huo, Mhandisi Patrick Rambika, Serikali hutumia kati ya sh. milioni 400 hadi 500 kila mwaka kuondoa mchanga unaoziba eneo la daraja hilo ili kuruhusu maji kupita bila kuathiri miundombinu hiyo. Hata hivyo, wakati mwingine upatikanaji wa fedha huwa changamoto na kuongeza hatari kwa uimara wa daraja hilo.


Akiwa eneo la Magoweko, wilayani Gairo, Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi juhudi ambazo zimefanywa na Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.


Aliwasisitiza wakazi hao watunze amani kwani ndiyo mtaji wa uhai wao. “Gairo kukiwa na amani watu wa kwanza kunufaika ni wanaGairo wenyewe. Kukiwa na uvunjifu wa amani, watu wa kwanza kuathirika ni wanaGairo wenyewe na amani ikipotea inahatarisha uhai wetu.”

“Kila ninakopita ninawakumbushia Watanzania kuwa mtaji wa kwanza wa kufanya shughuli yoyote ni uhai Mungu aliotupatia. Mtaji wa pili wa kufanya shughuli yoyote unayoiwaza ni amani katika eneo lako ulipo.”

No comments:

Post a Comment