
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM — Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Wakili Patrick Kipangula, amesema uhuru wa uhariri ni nguzo muhimu katika taaluma ya habari na unapaswa kulindwa ili vyombo vya habari viweze kutekeleza majukumu yake kwa weledi, uwajibikaji na kwa maslahi ya umma.
Akizungumza Mei 26, 2026 katika mahojiano maalum yaliyofanyika katika Ofisi za JAB jijini Dar es Salaam, Wakili Kipangula alisema hakuna mtu anayepaswa kuingilia maamuzi ya uhariri wa chombo cha habari, awe ni chanzo cha taarifa, mmiliki wa chombo, mwanasiasa au mtu mwingine yeyote mwenye maslahi binafsi.
Alisema uhuru huo unapaswa kuendana sambamba na uwajibikaji wa kitaaluma, huku akisisitiza kuwa maadili ya taaluma ya habari yanamtaka mwandishi kufanya kazi kwa uadilifu, bila upendeleo na kuhakikisha taarifa zote zinathibitishwa kabla ya kuchapishwa au kurushwa.
“Ukweli ndio mlinzi wa taaluma ya habari. Mwandishi anatakiwa kutoa taarifa ambazo amezithibitisha na ana uhakika nazo kwa sababu jamii inategemea kupata taarifa sahihi na kwa wakati ili iweze kufanya maamuzi sahihi kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo,” amesema Wakili Kipangula.
Aidha, alisema waandishi wa habari wana nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye uelewa, mshikamano na maendeleo, hivyo ni muhimu kutumia uhuru wa habari kwa kuzingatia sheria, maadili ya taaluma pamoja na kuheshimu haki na uhuru wa wengine kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.
Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Bw. Deodatus Balile, alisema uhuru wa vyombo vya habari utakuwa na maana halisi pale vyombo hivyo vitakapokuwa na uwezo wa kiuchumi wa kujiendesha bila kutegemea ushawishi wa nje.
“Uhuru wa vyombo vya habari utakuwa uhuru wa kweli pale vyombo vya habari vitakapokuwa na nguvu ya kiuchumi,” amesema Balile.

No comments:
Post a Comment