MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA JWTZ YAFIKIA ASILIMIA 92 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 19, 2026

MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA JWTZ YAFIKIA ASILIMIA 92



Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imesema matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kambi zake zinazohudumia zaidi ya watu 100 yamefikia asilimia 92, huku Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) likifikia asilimia 100 katika matumizi ya nishati hiyo.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Rhimo Nyansaho, amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi na utunzaji wa mazingira.

Dkt. Nyansaho amesema taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara hiyo zimeendelea kufanya maboresho katika matumizi ya nishati safi ambapo Shirika la Mzinga limefikia asilimia 98 ya matumizi ya nishati safi ya kupikia huku Tanzania Automotive Technology Center nalo likifikia asilimia 98.

Amesema Wizara kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeendelea kutekeleza mkakati wa matumizi ya nishati safi katika kambi zote za JKT nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, shughuli zilizotekelezwa ni pamoja na utengenezaji wa mashine za kuzalisha mkaa mbadala, ujenzi wa miundombinu ya mitambo ya gesivunde (biogas) katika baadhi ya vikosi vya JKT pamoja na kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu utengenezaji wa mkaa banifu katika kambi mbalimbali.

Mbali na matumizi ya nishati safi, Dkt. Nyansaho amesema Wizara imeendelea kuchukua hatua za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya jeshi yenye misitu ya asili kwa kuyakinga dhidi ya uvamizi wa shughuli za kibinadamu pamoja na kuendelea kupanda miti mipya.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara na taasisi zake zimefanikiwa kupanda miti mipya 209,794 katika kambi mbalimbali za jeshi nchini.

Aidha, amesema Wizara imeendelea na upimaji pamoja na uwekaji wa alama za mipaka katika maeneo ya jeshi yenye misitu na ardhi oevu, hatua ambayo imepunguza uvamizi, uharibifu wa mazingira na migogoro ya ardhi inayotokana na shughuli za kibinadamu kama uchomaji mkaa, ukataji miti, uchimbaji madini, kilimo na ufugaji. 



No comments:

Post a Comment