WIZARA YA ULINZI YAOMBA TRILIONI 4.28 KWA BAJETI YA 2026/2027 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, May 19, 2026

WIZARA YA ULINZI YAOMBA TRILIONI 4.28 KWA BAJETI YA 2026/2027



Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA


Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa imeomba jumla ya Shilingi trilioni 4.28 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo katika mwaka wa fedha 2026/2027, fedha zitakazotumika kuimarisha uwezo wa majeshi, kuboresha ustawi wa wanajeshi pamoja na kuendeleza miradi ya kimkakati ya Taifa.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2026, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, amesema kati ya fedha hizo, Shilingi trilioni 3.85 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida huku Shilingi bilioni 426.53 zikitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Dkt. Nyansaho amesema Fungu 38 - NGOME linatarajiwa kutengewa Shilingi trilioni 3.19 kwa matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 54.86 kwa maendeleo, huku Fungu 39 - Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) likitengewa Shilingi bilioni 626.27 kwa matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 19.92 kwa maendeleo.

Aidha, amesema Fungu 57 ambalo ni Wizara, linatarajiwa kutengewa Shilingi bilioni 35.55 kwa matumizi ya kawaida pamoja na Shilingi bilioni 351.73 kwa ajili ya maendeleo.

Katika mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri huyo amesema Wizara itaelekeza nguvu katika kuimarisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kulipatia zana na vifaa vya kisasa vya kijeshi, mifumo ya mawasiliano ya kiteknolojia pamoja na kuendeleza rasilimali watu.

Pia amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi kupitia huduma za afya, makazi, mafunzo, mazoezi pamoja na matengenezo ya vifaa na zana za kijeshi ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.

Kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Nyansaho amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya JKT ili liweze kupokea vijana wengi zaidi watakaopata mafunzo ya awali ya kijeshi sambamba na stadi mbalimbali za kazi.

Vilevile, amesema Serikali itaendelea kuimarisha Jeshi la Akiba pamoja na kulinda na kuendeleza miradi ya kimkakati yenye maslahi mapana kwa Taifa.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Wizara imepanga kuimarisha mashirika na taasisi za utafiti wa masuala ya kijeshi pamoja na kuanzisha viwanda vipya vya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa kwa matumizi ya kijeshi na kiraia kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Amesema Serikali pia itaendelea kuimarisha ushirikiano na United Nations, African Union, Southern African Development Community pamoja na East African Community katika masuala ya ulinzi na usalama wa kikanda.

Aidha, amesema Wizara itaendelea kushirikiana na mamlaka za kiraia katika kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali kwa maslahi ya wananchi na Taifa kwa ujumla.



No comments:

Post a Comment