Na. Mwandishi Wetu- Dodoma
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Bi. Albina Mtumbuka, amelipongeza na kulishukuru Shirika la Maendeleo la Habitat for Humanity Tanzania kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa vyoo vya kisasa na maeneo ya kunyonyeshea watoto katika minada ya Bahi na Kigwe wilayani humo.
Bi. Mtumbuka amesema kuwa mradi huo umeleta faraja kubwa kwa wananchi wanaotumia maeneo hayo ya minada kutokana na umuhimu wake katika kuboresha huduma za usafi na mazingira.
“Ni Furaha kubwa sana kwa wadau wetu wa Habitat for Humanity Tanzania kwa kutuletea mradi mzuri wa vyoo vya kisasa na maeneo ya kunyonyeshea watoto. Hakika huu mradi umekuwa ni faraja kwenye eneo hili. Na ikizingatiwa kwamba hii ni eneo la minada ambalo linachukua watu wa makundi mbalimbali. Kwenye hili eneo tuna wafugaji, kuna wanawake, kuna vijana. Wazee wote wanafika ili waweze kupata huduma,” amesema Bi. Mtumbuka.
Ameyasema hayo Aprili 28, 2026 mara baada ya kutembelea miradi ya vyoo vya kisasa inayotekelezwa katika minada ya Bahi na Kigwe, ambapo miradi hiyo miwili inagharimu jumla ya shilingi milioni 120 huku kila mradi ukigharimu shilingi milioni 60.
Aidha, amebainisha kuwa awali walikuwa na choo ambacho hakikukidhi mahitaji ya wananchi, lakini kupitia ufadhili wa Habitat Tanzania wamefanikiwa kupata choo bora na imara.
“tulikuwa na choo ambacho kilikuwa hakijatutolea. Lakini sasa hivi nipende kuwashukuru sana Habitat Tanzania kwa kutupa ufadhili na kutujengea choo bora na imara. Nina hakika huu sio mwisho bali itakuwa ni mwanzo wa kujenga vyoo kama hivi katika maeneo mengi ya minada wilayani kwetu Bahi,” amesema Bi. Mtumbuka.
Pia ameongeza kuwa wanaendelea kuwakaribisha wadau hao pamoja na kuwashukuru kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa wananchi wa Wilaya ya Bahi.
Awali akizungumza katika semina na wanufaika wa miradi hiyo, Mkurugenzi wa Miradi wa Shirika la Habitat for Humanity Tanzania, Bw. John Massenza, amesema kuwa sera ya Habitat inalenga kuboresha makazi ya wananchi hususan wanaoishi katika mazingira duni na wenye kipato cha chini.
Bw. Massenza amesema kuwa kupitia mradi huo wamefanikiwa kuboresha mazingira ya usafi na afya kwa watumiaji wa minada hiyo, jambo ambalo litasaidia kupunguza athari za magonjwa pamoja na kuongeza tija katika shughuli za kiuchumi.
Aidha, amebainisha kuwa kupungua kwa msongamano na muda wa kusubiri huduma kutawawezesha wafanyabiashara na wananchi kutumia muda mwingi zaidi katika uzalishaji na biashara, hali itakayosaidia kuongeza kipato chao.
Pia ameongeza kuwa Habitat for Humanity Tanzania imeanzisha mfuko wa jamii wenye lengo la kusaidia kaya zenye kipato cha chini kuboresha makazi yao.











No comments:
Post a Comment