Mshumaa wa upendo na matumaini wawashwa ALMC kwa wagonjwa tanzania - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, May 13, 2026

Mshumaa wa upendo na matumaini wawashwa ALMC kwa wagonjwa tanzania

Na Mwandishi Wetu, Arusha

HOSPITALI ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) chini ya menejimenti ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) wamefanikuwa kutoa huduma za matibabu bure kwa zaidi ya watu 2,000 kuelekea kilele cha maadhimisho ya wauguzi duniani.

Hospitali hizo pia zimekuwa wadhamini wakuu wa Maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika jijini Arusha, yakihusisha shughuli mbalimbali za kijamii pamoja na utoaji wa huduma za matibabu bure kwa wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maadhimisho hayo, Dk Saleh Hamisi Mwinchete ambaye ni Daktari Bingwa wa Moyo pamoja na Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali ya ALMC, alisema maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila tarehe 15 Mei kila mwaka ikiwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa mwanzilishi wa huduma za uuguzi duniani Florence Nightingale, yaliwakutanisha wauguzi kutoka maeneo mbalimbali nchini katika viunga vya Hospitali ya ALMC.

Alisema kabla ya kufikia kilele cha maadhimisho hayo, wauguzi pamoja na madaktari bingwa walitoa huduma za matibabu bure kwa wakazi wa jiji la Arusha kupitia vituo maalum vilivyowekwa katika Hospitali ya ALMC na Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC).

Alisema zaidi ya wananchi 1,400 walipata huduma mbalimbali za uchunguzi wa afya hususan magonjwa yasiyoambukiza, huku wauguzi 600 nao wakinufaika na huduma hizo, na kufanya jumla ya watu 2,000 kufaidika na huduma za matibabu bure zilizotolewa na Arusha Lutheran Medical Centre chini ya menejimenti ya JKCI.

Alisema lengo la huduma hizo ni kuwasaidia wananchi kufahamu hali ya afya zao kupitia uchunguzi wa mapema wa presha ya damu, kiwango cha sukari, mapigo ya moyo pamoja na viashiria vingine muhimu vya magonjwa yasiyoambukiza.

Alisema wananchi wengi hupata madhara makubwa ya magonjwa ya moyo kutokana na kutofanya uchunguzi mapema na kutofahamu viwango vya afya zao.

“Tunataka wananchi wajue namba zao. Kufahamu presha yako, kiwango cha sukari pamoja na hali ya afya ya moyo wako ni hatua muhimu ya kujikinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Dk. Mwinchete.

Aidha, alisema katika maadhimisho hayo pia kulifanyika tukio maalum la kuwasha mshumaa lililofanyika katika viunga vya Hospitali ya ALMC kwa mara ya kwanza katika historia ya maadhimisho hayo jijini Arusha. Tukio hilo lilikuwa ishara ya upendo, matumaini na amani kwa wagonjwa wanaopatiwa huduma katika hospitali mbalimbali nchini.

Baada ya kuwashwa, mshumaa huo wa upendo na matumaini ulipelekwa katika wodi mbalimbali za wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo, ambapo wauguzi walitembelea wagonjwa na kutoa zawadi maalum kama sehemu ya kuwafariji na kuwapa moyo katika kipindi cha matibabu yao

Baada ya zoezi hilo, wauguzi wote waliongozwa na bendi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika maandamano maalum kuelekea Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Arusha (AICC), ambako walipokelewa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo pamoja na viongozi mbalimbali wa sekta ya afya.

Dkt. Mwinchete alisema wauguzi wana mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwani zaidi ya asilimia 60 ya huduma zote anazozipata mgonjwa hospitalini hutolewa kupitia kada hiyo.

Kutokana na umuhimu huo, alisema JKCI pamoja na ALMC zimeendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wauguzi kupitia mafunzo ya kitaaluma, huduma kwa wateja na mbinu bora za utoaji huduma ili kuongeza ubora wa huduma kwa wagonjwa.

Aidha, alisema taasisi hizo zimeanza maandalizi kuelekea mashindano ya Africa Cup of Nations ambapo ALMC inatarajiwa kuwa miongoni mwa vituo vya kutoa huduma za dharura kwa wageni, mashabiki na washiriki wa mashindano hayo sambamba na kutoa mafunzo maalumu kwa wauguzi na madaktari kuhusu utoaji wa huduma za dharura.

Kwa mujibu wa Dkt. Mwinchete, maandalizi hayo yanahusisha mafunzo maalum kwa wauguzi na wataalamu wengine wa afya ili kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kutoa huduma za afya zenye viwango vya kimataifa wakati wa mashindano hayo makubwa ya bara la Afrika.

No comments:

Post a Comment