Serikali imewahakikishia wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga kuendelea kuboresha mazingira yao ya kufanyia biashara, ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kukuza uchumi jumuishi na kuongeza fursa za ajira nchini.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), wakati akihutubia katika Mkutano Mkuu wa Baraza la Machinga uliofanyika katika Viwanja vya Mwenge, Kinondoni jijini Dar es Salaam, uliolenga kujadili mafanikio ya wamachinga katika siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania madarakani pamoja na kuweka mikakati ya kulijenga Taifa.
Mhe. Mhandisi Munde alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara wadogo ili waweze kukuza mitaji yao na hatimaye kupanda daraja na kuwa wafanyabiashara wakubwa.
“Tunataka kuwaona mnapiga hatua kutoka biashara ndogondogo hadi kuwa wawekezaji wakubwa na Serikali yenu inatambua mchango wenu katika uchumi na itaendelea kuwaunga mkono,” alisema Mhe. Mhandisi Munde.
Aidha Mhe. Mhandisi Munde, alisisitiza kuwa maoni na mapendekezo yatokanayo na mkutano huo yatasaidia kuboresha sera na mifumo ya biashara nchini, sambamba na utekelezaji wa falsafa ya 4Rs (Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya) inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Aliongeza kuwa Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kurasimisha sekta isiyo rasmi, hatua itakayowezesha wafanyabiashara kupata fursa zaidi za mikopo nafuu, mafunzo na huduma nyingine muhimu za kiuchumi ikiwemo maeneo mazuri zaidi ya kufanya biashara kwa utulivu.
“Ni muhimu mkakubali kufanya kazi katika maeneo mtakayotengewa ili kurahisisha Serikali yenu kuwekeza miundombinu na huduma muhimu katika maeneo hayo na Pia, taasisi kama TRA na benki zitaendelea kuboresha huduma zao ili ziwe rafiki kwa wafanyabiashara wadogo,” alisisitiza Mhe. Mhandisi Munde.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, pongezi za dhati kwa Wizara ya Fedha pamoja na taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa wafanyabiashara wadogo, ikiwemo juhudi za Mamlaka ya Mapato Tanzania -TRA katika kuonyesha uwajibikaji na mafanikio makubwa ya ukusanyaji mapato.
“Kwa dhati nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono na jitihada zake za kufungua fursa za kiuchumi na kuimarisha miundombinu ya biashara, ikiwemo ujenzi wa masoko na maboresho ya maeneo ya biashara katika Wilaya ya Kinondoni, hasa kwa kutupa masoko zaidi ya 24 yakiwemo makubwa kama Tandale, na kuendelea kuboresha masoko mengine na kuongeza vibanda ili kuwawezesha wafanyabiashara wengi zaidi kufanya shughuli zao katika mazingira bora na salama” alisema Bw. Mtambule
Naye Mwenyekiti wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Taifa, Bw. Ernest Mtondo alisema kuwa, Wamachinga wanatambua na wanathamini juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara, pamoja na jitihada za kuimarisha zaidi mifumo ya hifadhi ya jamii kwa wajasiriamali hao.
Bw. Mtondo aliishukuru Wizara ya Fedha kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuanza kuweka mazingira rafiki ya biashara, ikiwemo ujenzi wa mahema katika maeneo maalum ambayo yatabeba zaidi ya wamachinga 300, hatua ambayo imeanza kuleta utulivu na heshima kwa shughuli za wamachinga.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) Taifa, Bw. Joseph Mwanakijiji, amesema kuwa kuanzishwa kwa shirikisho hilo kumelenga kuwaunganisha wamachinga na wafanyabiashara ndogondogo nchini kote, huku likikuza ushirikiano thabiti kati yao na Serikali.
Bw. Mwanakijiji alisema kuwa kupitia SHIUMA, wamachinga wameanza kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za kifedha, pamoja na kupendekeza na kurasimisha maeneo rafiki ya biashara.
“Tayari kumekuwepo na maboresho makubwa ikiwemo ujenzi wa masoko maalum kama Machinga Complex Dodoma, kuimarika kwa mahusiano na Serikali, pamoja na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara katika maeneo mbalimbali kama Mwenge na tunaahidi kuongeza ushirikiano na TRA katika ukusanyaji wa mapato pamoja na kuwahamasisha zaidi wamachinga kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii kama NSSF ili kujenga ustawi wao wa baadaye” alisema Bw. Mwanakijiji.







No comments:
Post a Comment