WAKAZI WA BAGAMOYO WAHIMIZWA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 11, 2026

WAKAZI WA BAGAMOYO WAHIMIZWA KUTUMIA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Wakazi wa Wilaya ya Bagamoyo wameaswa kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa mazingira kwa kutumia nishati safi na salama ya kupikia kwa kutumia majiko banifu.

Rai hiyo imetolewa Mei 7, 2026 na Katibu Tawala wa Wilaya ya Bagamoyo, Stella Msofe, wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku.

Mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni sehemu ya mwendelezo wa juhudi za Serikali za kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wenye la kuongeza upatikanaji na matumizi kwa asilimia 80 ifikapo mwaka 2034.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Bi. Msofe alisema matumizi ya majiko banifu yatasaidia kupunguza utegemezi wa nishati zisizo salama kwa mazingira na afya za wananchi na kupunguza gharama za matumizi ya nishati majumbani na katika shughuli za biashara ya chakula.

“Tuhakikishe tunapata majiko haya kwa sababu yanatunza mazingira yetu. Tuunge mkono juhudi za Rais wetu katika kuhakikisha kila Mtanzania anatumia nishati safi na salama ya kupikia,” alisema Bi. Msofe.
Katika mradi huo, majiko banifu 1,522 yanatarajiwa kuuzwa kwa wananchi wa Bagamoyo kwa bei ya ruzuku ya shilingi 11,200 kwa kila jiko badala ya bei halisi ya shilingi 56,000.

Kwa upande wake, Mtoa huduma kampuni ya L'S Solution Ltd inayosambaza majiko hayo wilayani Bagamoyo, imeeleza kuwa teknolojia iliyotumika katika utengenezaji wa majiko hayo inalenga kupunguza uchafuzi wa mazingira pamoja na matumizi makubwa ya gharama za nishati.

Baadhi ya wananchi wa Bagamoyo wameipongeza Serikali kwa kuwaletea teknolojia hiyo, wakisema itawasaidia katika matumizi ya kila siku majumbani pamoja na shughuli zao za biashara, hususan kwa mama lishe na baba lishe. 

No comments:

Post a Comment