PPRA YAWAHIMIZA MAKUNDI MAALUM KUNYAKUA ASILIMIA 30 YA ZABUNI ZA SERIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, June 27, 2026

PPRA YAWAHIMIZA MAKUNDI MAALUM KUNYAKUA ASILIMIA 30 YA ZABUNI ZA SERIKALI


MAMLAKA ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imewahimiza vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu kujisajili kwa wingi katika Mfumo wa Kitaifa wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Kielektroniki (NeST) ili kunufaika na fursa za zabuni zinazotolewa na Serikali.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa PPRA, Dennis Simba, wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyohitimishwa jijini Dodoma.

Simba amesema Serikali imeweka mazingira rafiki ya ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya mwaka 2023 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2024.

Ameeleza kuwa sheria hiyo imezitaka taasisi zote za umma kutenga asilimia 30 ya bajeti zao za ununuzi kwa ajili ya makundi maalum ya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu, hatua inayolenga kuongeza ushiriki wao katika biashara za Serikali.

"Tunamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake yaliyowezesha kupitishwa kwa sheria hii ambayo imefungua milango ya ushiriki mpana wa wananchi katika biashara na Serikali. Hii ni fursa muhimu kwa Watanzania," amesema Simba.

Amebainisha kuwa hadi sasa zaidi ya vikundi 8,700 vimejisajili katika mfumo wa NeST, huku thamani ya zabuni zilizotolewa kwa makundi maalum ikifikia takribani shilingi bilioni 50 na mikataba iliyosainiwa kuzidi shilingi bilioni 45.

Aidha, amesema PPRA kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Ofisi ya Rais imeendelea kutoa elimu nchini kote ili kuongeza uelewa kuhusu fursa hizo na namna ya kuzitumia.

Pia amewataka wanahabari kuendelea kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kujisajili katika mfumo wa NeST, akisisitiza kuwa hakuna ubaguzi katika upatikanaji wa zabuni za Serikali.

Kwa upande mwingine, amewaalika wadau wa sekta binafsi kushiriki Kongamano la Ununuzi wa Umma litakalofanyika jijini Arusha mwishoni mwa Julai, ambapo mafanikio, changamoto na maboresho ya mfumo wa ununuzi wa umma yatajadiliwa.

No comments:

Post a Comment