WAZIRI WA FEDHA AIAGIZA NBAA KUANDAA WATAALAMU WENYE KUKIDHI MAHITAJI YA MAENDELEO YA TAIFA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, May 11, 2026

WAZIRI WA FEDHA AIAGIZA NBAA KUANDAA WATAALAMU WENYE KUKIDHI MAHITAJI YA MAENDELEO YA TAIFA

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akiagana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia Temu, walipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa NBAA, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), akizungumza jambo wakati wa kikao chake na uongozi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), ukiongozwa na Mwenyekiti wake wa Bodi ya Wakurugenzi, CPA. Prof. Sylvia Temu (Hayupo pichani), kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, ambapo aliiagiza Bodi hiyo kuhakikisha kuwa sekta ya uhasibu nchini inajengwa katika misingi imara ya maadili ili kuzalisha wataalamu wenye uadilifu, uwajibikaji na weledi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Sylvia Temu, akizungumza jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), na uongozi wa NBAA, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, ambapo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA. Prof. Siasa Mzenzi, akizungumza jambo wakati wa kikao cha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (hayupo pichani), na uongozi wa NBAA, kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) (Katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Sylvia Temu (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA. Prof. Siasa Mzenzi, wakiwa katika picha ya pamoja walipokutana na kufanya mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam.


(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)



Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), ameiagiza Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), kuhakikisha kuwa sekta ya uhasibu nchini inajengwa katika misingi imara ya maadili ili kuzalisha wataalamu wenye uadilifu, uwajibikaji na weledi unaokidhi mahitaji ya maendeleo ya Taifa.

Mhe. Balozi Omar alitoa maagizo hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Bodi hiyo ulioongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NBAA, CPA Prof. Sylvia Temu, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, ambapo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

Alisema Serikali inaendelea kutegemea taaluma ya uhasibu kama nguzo muhimu katika kuhakikisha usimamizi bora wa fedha, uwazi wa taarifa za kifedha pamoja na kuimarisha imani ya wananchi na wawekezaji katika mifumo ya kiuchumi nchini.

“Ni muhimu sana kwa NBAA kuhakikisha kuwa wataalamu wa kada ya uhasibu wanalelewa katika misingi ya maadili, uaminifu na uzalendo kwa sababu taaluma hii inagusa moja kwa moja usimamizi wa rasilimali za Taifa,” alisema Mhe. Balozi Omar.

Aidha, aliipongeza NBAA kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua katika kuboresha taaluma hiyo ikiwemo matumizi ya teknolojia ya kisasa katika usimamizi wa taarifa za fedha pamoja na kuendelea kusajili wahasibu na kampuni za ukaguzi nchini.

Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Sylvia Temu, alisema Taasisi hiyo imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kusimamia taaluma ya uhasibu na ukaguzi wa hesabu nchini huku ikiweka mkazo katika kujenga wataalamu wenye viwango vya kimataifa.

Alieleza kuwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026, NBAA imefanikiwa kusajili Wahasibu Wahitimu (CPA Graduate Accountants) 8,864, Wahasibu wa ngazi ya Associate 6,631 pamoja na Wahasibu wa ngazi ya Fellow 529.

Aidha, CPA Prof Temu alisema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, kampuni mpya 22 za ukaguzi pamoja na kampuni 19 za kihasibu zilisajiliwa huku wahasibu 271 wakisajiliwa rasmi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), CPA Prof. Siasa Mzenzi, alisema kuwa hivi sasa imekamilisha kutengeneza Mfumo wa kisasa wa ukusanyaji wa taarifa za fedha unaojulikana kama NBAA-VN ambao tayari umekusanya zaidi ya taarifa za fedha 11,000 kutoka kampuni mbalimbali nchini, ambao utasaidia kudhibiti udanganyifu wa taarifa za fedha, kuzuia kampuni hewa za ukaguzi na kuongeza uwazi katika sekta ya fedha.

“Tunataka kuhakikisha taarifa za fedha nchini zinakuwa salama, sahihi na zinapatikana kwa urahisi kwa taasisi husika za Serikali na Taasisi nyingine za sekta binafsi zikiwemo benki,” alisema CPA. Prof. Mzenzi

CPA. Prof Mzenzi aliongeza kuwa, zaidi ya wahasibu 2,149 wamepatiwa mafunzo kuhusu viwango vya kimataifa vya taarifa za fedha za uendelevu (Sustainability Financial Reporting), hatua inayolenga kuandaa wataalamu wanaozingatia mazingira, uwajibikaji na mabadiliko ya tabianchi katika utoaji wa taarifa za kifedha.

No comments:

Post a Comment