
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Wizara ya Afya imeomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi trilioni 1.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutekeleza vipaumbele mbalimbali vya sekta ya afya nchini, ikiwemo kuboresha huduma za matibabu, utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha hospitali na taasisi zake.
Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa amesema wizara inaomba kuidhinishiwa kiasi cha Shilingi 1,800,262,058,000.00 kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Mchengerwa amesema kati ya fedha hizo, Shilingi 652,236,871,000.00 sawa na asilimia 36 ya bajeti yote zitatumika kwa matumizi ya kawaida, huku kiasi cha Shilingi 1,148,025,187,000.00 sawa na asilimia 64 kikielekezwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Amefafanua kuwa katika fedha za matumizi ya kawaida, kiasi cha Shilingi 516,323,356,000.00 kimetengwa kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa Wizara, hospitali pamoja na taasisi zilizo chini yake, huku Shilingi 135,913,515,000.00 zikitengwa kwa matumizi mengineyo.
Kwa upande wa miradi ya maendeleo, Waziri huyo amesema Shilingi 789,458,609,000.00 ni fedha za ndani huku Shilingi 358,566,578,000.00 zikiwa ni fedha kutoka vyanzo vya nje kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali ya afya nchini.
Aidha, Wizara hiyo imekadiria kukusanya maduhuli ya Shilingi 747,200,091,299.81 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kupitia Wizara, taasisi na hospitali zake.
Kwa mujibu wa Waziri Mchengerwa, kati ya fedha hizo Shilingi 76,195,850,735.53 zinatarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo vya ndani vya Makao Makuu ya Wizara, Shilingi 165,804,149,264.47 kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa na zaidi ya Shilingi 505 bilioni kutoka Taasisi, Hospitali ya Taifa, hospitali maalum pamoja na hospitali za kanda.
Waziri huyo amesema fedha zinazoombwa zitawezesha Wizara ya Afya kuendelea kuboresha huduma za afya, kuimarisha miundombinu ya matibabu, upatikanaji wa vifaa tiba pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

No comments:
Post a Comment