BAJETI YA 2026/27 KUFUNGUA UKURASA WA DIRA 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 10, 2026

BAJETI YA 2026/27 KUFUNGUA UKURASA WA DIRA 2050


Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar,akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 10,2026 jijini Dodoma kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 inayotarajiwa kusomwa kesho Juni 11,2026 bungeni Dodoma.


Na Mwandishi Wetu , Dodoma


SERIKALI inatarajia kutumia Sh trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa lengo la kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Juni 10,2026 kuhusu Bajeti ya Serikali inayotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amesema bajeti hiyo ni ya kihistoria kwa kuwa ndiyo ya kwanza kutekeleza kwa vitendo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Bajeti hii inakuja katika kipindi muhimu ambapo Taifa limeanza safari ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Dhamira yetu ni kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi, endelevu na wenye manufaa kwa wananchi wote,” amesema.

Amesema bajeti hiyo imeelekezwa katika kuimarisha ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira, kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kuboresha ustawi wa wananchi kupitia huduma mbalimbali za kijamii.

Kwa mujibu wa Waziri Omar, maeneo yatakayopewa kipaumbele ni pamoja na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), uboreshaji wa miundombinu ya barabara, upanuzi wa huduma za maji na nishati pamoja na uwekezaji katika sekta za elimu, afya na maendeleo ya ujuzi.

Amesema Serikali inalenga kukusanya Sh trilioni 46.8 kutoka vyanzo vya ndani, hatua inayoonesha kuimarika kwa uwezo wa nchi kujitegemea katika kugharamia maendeleo yake.

Waziri huyo amesema utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2025/26 umeendelea kuleta matokeo chanya kutokana na mwenendo mzuri wa ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Akizungumzia maboresho ya kodi, ada na tozo, alisema Serikali ilipokea mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali, ambapo kati ya hayo, 125 yalikubaliwa moja kwa moja na 121 yakafanyiwa maboresho kabla ya kupitishwa.

Amesema lengo la maboresho hayo ni kuchochea ukuaji wa uchumi, kuvutia uwekezaji, kuongeza wigo wa walipa kodi na kuondoa baadhi ya changamoto zilizokuwa zikikabili walipa kodi.

Aidha, amesema maandalizi ya maboresho hayo yalihusisha ushiriki wa wadau mbalimbali kupitia Kamati ya Wataalam ya Maboresho ya Kodi na Kamati ya Ushauri ya Ngazi ya Juu ya Think Tank.

Waziri Omar amewataka wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati huku Serikali ikiendelea kuimarisha usimamizi wa fedha za umma ili kuhakikisha zinatumika kwa ufanisi.

Pia aliwahimiza Watanzania kufuatilia kwa karibu hotuba ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 itakayowasilishwa bungeni leo ili kupata ufahamu wa kina wa vipaumbele na mwelekeo wa maendeleo ya taifa katika mwaka mpya wa fedha.

No comments:

Post a Comment