UJUMBE WA TANZANIA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA KUZUIA UTUMIKISHWAJI WA MTOTO GENEVA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, June 10, 2026

UJUMBE WA TANZANIA WASHIRIKI MAADHIMISHO YA KUZUIA UTUMIKISHWAJI WA MTOTO GENEVA

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Bw. Gilbert Houngbo akihutubia wakati  wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tempus, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9 Juni, 2026, Geneva, Uswizi.

*************

Na: OWM (KAM) - Geneva, Uswizi

Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeungana na mataifa mengine katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika tarehe 9 Juni, 2026 katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, Geneva, Uswisi.

Aidha, ujumbe huo wa Tanzania uliongozwa na Kamishna wa Kazi, Suzan Mkangwa ambaye aliambatana na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Dkt. Yose Joseph Mlyambina, Kamishna wa Kazi Zanzibar, Rashid Khamis Othman, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Wataalamu na Wawakilishi wa Waajiri (ATE) pamoja na Wawakilishi kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA).

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO), Gilbert F. Houngbo ametoa wito kwa jamii ya Kimataifa na Wadau wa Utatu kutekeleza kwa vitendo Mipango na Maadhimio ya Mkutano wa Marrakesh uliofanyika nchini Morocco, Februari 2026 kwa lengo la kupinga utumikishwaji wa Mtoto.

Vilevile, alisisitiza juu ya jitihada za makusudi zinazotakiwa kuchukuliwa na nchi wanachama wa ILO, katika kukuza kazi za staha na utekelezaji wa sera ya elimu bure.

Kwa upande wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira na Mahusiano imeendelea kudhihirisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kazi na ajira, hasa hatua madhubuti zilizochukuliwa katika kutokomeza ajira za watoto nchini ni kama zifuatazo:- Utekelezaji wa Mradi wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Brazil kwa kushirikiana na ILO mradi huo umefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutoa elimu kuhusu utumikishwaji wa mtoto na madhara yake.

Pia, kuhuishwa kwa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Utumikishwaji wa Mtoto 2024/25–2028/29, unaolenga kuunganisha nguvu za wadau wote wa maendeleo, mashirika ya kiraia na jamii kwa ujumla. Kadhalika, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya Haki Kazini kupitia Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi, na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA). Vyombo hivi vimekuwa vikitimiza vyema wajibu wake wa kutafsiri sheria na kutoa haki, hususani ulinzi kwa mtoto; Kuadhimisha Siku ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto Kitaifa kila tarehe 12 Juni. Wadau kutoka Tanzania Bara na Zanzibar hushiriki na kupokea mikakati ya Serikali ya kukabiliana na tatizo hili; pamoja na Kutoa elimu kwa Umma kwa kuwa utumikishwaji wa mtoto ni jukumu la jamii nzima, hivyo ushirikiano baina ya Wizara, wadau wa maendeleo, kaya, na kila mwananchi unahitajika ili kufafanua tafsiri ya utumikishwaji wa mtoto, kazi za shuruti, na kazi hatarishi kwa afya na maendeleo ya mtoto.

Siku ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto uadhimishwa kila mwaka tarehe 12 Juni na Shirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na nchi wanachama kwa lengo la kuhamasisha nguvu ya pamoja baina ya Serikali, Vyama vya Waajiri, na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi katika kukuza ajira zenye staha na kutokomeza utumikishwaji wa watoto unaowanyima fursa za kijamii, hususan haki ya elimu.

Maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2026 yataongozwa na Kaulimbiu isemayo: “Red Card to Child Labour” ikimaanisha wito kwa wadau wote wa maendeleo kutoonesha uvumilivu wowote kwa vitendo vinavyochochea au kusababisha utumikishwaji wa mtoto katika sekta zote za kijamii na kiuchumi.
Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Bw. Gilbert Houngbo akihutubia wakati  wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tempus, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9 Juni, 2026, Geneva, Uswizi.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Yose Joseph Mlyambina (kushoto) Kamishna wa Kazi, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Bi. Suzan Mkangwa (kulia) na Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (katikati) wakifuatilia hotuba ya  Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Bw. Gilbert Houngbo wakati  wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Utumikishwaji wa Mtoto yaliyofanyika katika Ukumbi wa Tempus, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, tarehe 9 Juni, 2026, Geneva, Uswizi.


No comments:

Post a Comment