
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, amekabidhi hati za utambulisho kwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Algeria Mheshimiwa Abdelmadjid Tebboune katika hafla iliyofanyika kwenye Ikulu ya Algeria jijini Algiers, ikiwa ni ishara ya kuanza rasmi utekelezaji wa majukumu yake ya kibalozi.
Katika mazungumzo yao baada ya hafla hiyo, Mhe. Balozi Matinyi alimshukuru Mhe. Rais Tebboune, Serikali na watu wa Algeria kwa niaba ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kudumisha ushirikiano wa kindugu wa nchi hizi mbili ambao umedumu kwa zaidi ya miongo sita.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya mazungumzo na Mhe. Rais Tebboune, Balozi Matinyi alisema kwamba walijadiliana namna ya kusonga mbele baada ya kufikia mafanikio mazuri katika sekta za ulinzi na elimu ya juu ili kuhakikisha watu wa nchi hizi wananufaika pia katika sekta zingine muhimu.
Mhe. Balozi Matinyi alizitaja sekta walizojadiliana kwamba zinahitaji kufanyiwa kazi hivi sasa kuwa ni kilimo, viwanda, utengenezaji dawa, nishati, madini na utalii pamoja na kuongeza ushirikiano katika sekta za ulinzi, elimu ya juu, sayansi, teknolojia, utafiti na utamaduni ili kuboresha ushirikiano baina ya watu wa nchi zote mbili.
Aidha, Mhe. Rais Tebboune alisema wakati wa mazungumzo yao kwamba Algeria iko tayari kushirikiana na Tanzania katika sekta zote muhimu na itakuwa tayari kufikia makubaliano ya ushirikiano zaidi kupitia vikao vya pamoja na ziara za viongozi kama alivyopendekeza Mhe. Balozi Matinyi.
Mhe. Balozi Matinyi anakuwa balozi wa nne kuiwakilisha Tanzania nchini Algeria baada ya Mhe. Balozi Omari Yussuf Mzee (2017-2020), Mhe. Balozi Meja Jenerali Jacob Kingu (2020-2023) na Mhe. Balozi Imani Njalikai (2023-2026). Ubalozi wa Algiers huiwakilisha pia Tanzania katika nchi za Tunisia, Mauritania, Niger na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi (SADR).

No comments:
Post a Comment