Na. Mwandishi wetu, DODOMA
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Alimwoni Chaula, amefanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kidia, ambayo ni miongoni mwa barabara zinazoboreshwa kwa kiwango cha lami katikati ya Jiji la Dodoma.
Ujenzi wa barabara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dk. Samia Suluhu Hassan, ya kutaka halmashauri za majiji kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa barabara za mitaa.
Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Mstahiki Meya Chaula aliwataka wananchi kushiriki katika kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu. “Wananchi kwa pamoja tunapaswa kushirikiana katika kuzitunza barabara hizi kwa kufuata taratibu zilizowekwa. Wafanyabiashara waepuke kufanya biashara katika maeneo ya barabarani kwani hali hiyo huchangia uharibifu wa miundombinu hiyo” alisema Chaula.
Aliongeza kuwa halmashauri itaendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara kupitia viongozi mbalimbali wa maeneo husika kuhusu athari za kufanya shughuli za biashara kwenye hifadhi ya barabara.
Kwa upande wake, mfanyabiashara wa eneo hilo, Peter Moshi ameishukuru serikali kwa kutekeleza mradi huo akisema kuwa wananchi walikuwa wakisubiri kwa muda mrefu kuona barabara hiyo ikiboreshwa na kukamilika kwake kutarahisisha shughuli za biashara, kuongeza usafiri wa uhakika na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo jirani.
Barabara zinazotekelezwa katika mpango huo zina jumla ya urefu wa kilometa moja kila moja na zinagharimu takribani shilingi bilioni 1.9 kwa ujumla.








No comments:
Post a Comment