Dodoma Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dkt. Toba Nguvila, amepongeza matumizi ya mfumo wa kisasa wa Supervisory Control and Data Acquisition (SCADA) unaotumiwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA), akisema umeongeza uwazi na ufanisi katika usimamizi wa mafuta nchini.
Dkt. Nguvila alitoa pongezi hizo Juni 23, 2026, alipotembelea banda la PBPA katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma na kupata maelezo kuhusu namna mfumo huo unavyofanya kazi.
Alisema matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya mafuta yanaisaidia Serikali kufuatilia kwa karibu mwenendo wa mafuta yanayoingia nchini na kuhifadhiwa katika maghala mbalimbali, hivyo kudhibiti upotevu na kuongeza uwajibikaji.
“Ni jambo la kutia moyo kuona taasisi za umma zinatumia teknolojia za kisasa katika kuboresha usimamizi wa rasilimali za taifa. Mfumo huu unasaidia kuongeza uwazi na kuhakikisha mafuta yanayopokelewa yanafika katika maeneo yaliyokusudiwa,” alisema Dkt. Nguvila.
Akitoa maelezo kwa mgeni huyo, Mkaguzi wa Mafuta wa PBPA, Bw. Issa Khamis Mwitazy, alisema mfumo wa SCADA umechangia kwa kiasi kikubwa kudhibiti upotevu wa mafuta ambao kwa muda mrefu ulikuwa changamoto katika sekta hiyo.
Bw. Mwitazy alisema mfumo huo hulinganisha kiwango cha mafuta kilichopokelewa kutoka melini na kiwango kilichofika kwenye maghala, ambapo taarifa hutolewa mara moja endapo kutabainika tofauti yoyote ili hatua za haraka zichukuliwe.
Aidha, alisema mfumo huo unasoma na kufuatilia kwa wakati halisi ujazo wa mafuta kupitia mita za Serikali zilizopo katika bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, pamoja na kusoma kiwango cha mafuta kilichopo katika maghala ya kampuni za mafuta.
Kwa mujibu wa PBPA, matumizi ya mfumo wa SCADA ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi wa mafuta nchini na kuhakikisha sekta hiyo inaendeshwa kwa uwazi, ufanisi na tija zaidi.

No comments:
Post a Comment