
Rais wa Jamhuri ya Namibia, Mhe. Dkt. Netumbo Nandi-Ndaitwah, ametemebelea eneo la magomeni katika nyumba aliyowahi kuishi wakati wa harakati za ukombozi wa Namibia kupitia chama cha SWAPO.
Katika ziara hiyo ya kipekee iliyochanganya hisia za kumbukumbu na mshikamano wa kihistoria kati ya Tanzania na Namibia, Rais Nandi-Ndaitwah alipokelewa kwa furaha na majirani zake hao wa Magomeni, akiwemo mama Salehe na mtoto wa mama Salama ambao walimfahamu tangu alipokuwa akiishi eneo hilo akiwa mwakilishi wa harakati za ukombozi.
Akizungumza na wakazi hao, Rais huyo alitoa shukurani zake kwa Serikali na wananchi wa Tanzania kwa mchango wao mkubwa katika harakati za ukombozi wa Namibia, akisisitiza kuwa historia hiyo imejenga uhusiano imara na wa kudumu kati ya mataifa hayo mawili.
“Magomeni ni sehemu ya maisha yangu na historia ya taifa langu. Tanzania ilitupa hifadhi, upendo na nafasi ya kupigania uhuru wetu. Huu ni ushahidi wa urafiki wa kweli na mshikamano wa Afrika,” alisisitiza.
Baada ya mazungumzo hayo, Rais Nandi-Ndaitwah alitembea nyumba aliyowahi kuishi, akapata fursa ya kukumbuka maisha ya miaka hiyo ya mapambano, huku majirani hao wakishiriki kumbukumbu na furaha ya kukutana tena na kiongozi huyo akiwa amefika kuwasilimu katika nafasi yake mpya ya Urais.







No comments:
Post a Comment