Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imewahamasisha wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza kuchangia Mfuko wa Elimu wa Taifa ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia nchini.
Wito huo umetolewa na maafisa wa TEA katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma, ambapo taasisi hiyo inashiriki maonyesho kwa lengo la kutoa elimu kuhusu shughuli zake na mchango wa Mfuko wa Elimu wa Taifa katika maendeleo ya sekta ya elimu.
Akizungumza katika maonyesho hayo, Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa TEA, Eliafile Solla, alisema taasisi hiyo inayofanya kazi chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ina jukumu la kusimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa kwa kutafuta rasilimali fedha na vifaa pamoja na kuzitumia kuimarisha miundombinu ya elimu nchini.
Alisema maadhimisho hayo yameitoa fursa kwa TEA kukutana na wadau wake mbalimbali kwa wakati mmoja, wakiwemo wanufaika wa miradi ya elimu na wachangiaji wa maendeleo ya sekta hiyo kupitia mfuko huo.
“Tumeshiriki maonyesho haya ili kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutoa elimu kuhusu Mfuko wa Elimu wa Taifa, kazi zake, mafanikio yaliyopatikana na mipango ya baadaye ya kuboresha miundombinu ya elimu nchini,” alisema Solla.
Aliongeza kuwa kupitia mfuko huo, TEA imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji katika maeneo tofauti nchini.
Kwa upande wake, Afisa Usimamizi wa Miradi wa TEA, Joyce Minja, aliwataka wadau kujitokeza kuchangia mfuko huo akieleza kuwa mbali na kusaidia maendeleo ya elimu, wachangiaji hupata manufaa mbalimbali ikiwemo kutambuliwa kitaifa kwa mchango wao.
Minja alisema wachangiaji pia hupewa cheti maalumu cha utambuzi kinachojulikana kama Certificate of Education Appreciation, ambacho kinaweza kutumika kupata nafuu ya kodi kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Aliwahimiza wananchi kutembelea banda la TEA katika Viwanja vya Chinangali Park ili kupata elimu zaidi kuhusu miradi inayotekelezwa kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa na fursa zilizopo kwa wadau wanaotaka kushiriki katika maendeleo ya sekta ya elimu.
Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanaendelea jijini Dodoma yakikutanisha taasisi mbalimbali za umma zinazotoa huduma na elimu kwa wananchi.






No comments:
Post a Comment