UNCDF NA UNDP KUCHOCHEA UWEKEZAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, June 23, 2026

UNCDF NA UNDP KUCHOCHEA UWEKEZAJI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA TANZANIA

  


Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) wameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kusaidia upatikanaji wa fedha za uwekezaji zitakazochochea utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati nchini.

Ahadi hiyo imetolewa na Kiongozi wa UNCDF, Pradeep Kurukulasuriya akiwa ameambatana na Kiongozi wa UNDP, Shijeki Komatsubava, wakati wa kikao na Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, jijini Dodoma kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Salome Makamba amesema Serikali imeendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanahamia kwenye nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034. 

Amesema mwaka 2021 ni asilimia sita tu ya Watanzania waliokuwa wakitumia nishati safi ya kupikia, lakini kutokana na juhudi za Serikali, wadau wa maendeleo na sekta binafsi, kiwango hicho kimeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 28.

“Safari bado ni ndefu na inahitaji uwekezaji mkubwa pamoja na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Mhe. Salome Makamba.

Ameeleza kuwa, Serikali imeelekeza nguvu zaidi katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa wakati mmoja zikiwemo shule, vyuo, hospitali na hata majeshi, huku ikiendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Mhe. Salome Makamba amesema moja ya changamoto kubwa iliyopo ni upatikanaji wa rasilimali za kifedha zitakazowezesha wananchi na taasisi mbalimbali kupata teknolojia za nishati safi ya kupikia kwa urahisi zaidi, hususan katika maeneo ya vijijini ambako matumizi ya kuni na mkaa bado ni makubwa.

Kwa upande wake, Pradeep Kurukulasuriya amesema UNCDF ipo tayari kusaidia Tanzania kuvutia uwekezaji kupitia mifumo ya dhamana za mikopo, ruzuku za uwekezaji na mbinu nyingine za kifedha zinazolenga kupunguza hatari kwa wawekezaji na taasisi za fedha.

Amefafanua kuwa, Taasisi hiyo ina uzoefu wa kusaidia nchi mbalimbali kuvutia uwekezaji mkubwa kupitia mifumo ya ubunifu wa kifedha, ikiwemo matumizi ya dhamana za mikopo na fedha za kaboni, hatua ambayo inaweza kusaidia Tanzania kufikia malengo yake ya nishati safi ya kupikia kwa haraka zaidi.

"UNCDF iko tayari kufanya kazi kwa karibu na Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha pamoja na taasisi za fedha nchini ili kuandaa mpango maalumu wa kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya nishati safi ya kupikia". Amesema “Kurukulasuriya.

Kwa upande wake Shijeki Komatsubava amesema UNDP itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuweka mazingira wezeshi yatakayosaidia kuongeza uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia, hususan kwa wananchi wa maeneo ya vijijini na makundi yenye kipato cha chini.

Katika kikao hicho, pande hizo mbili zilijadiliana fursa za kutumia fedha za kaboni (carbon credits), kuimarisha ushiriki wa taasisi za fedha za ndani pamoja na kuandaa mifumo ya ubunifu wa kifedha itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Mhe. Salome ameishukuru UNCDF na UNDP kwa mchango wao katika kujenga uwezo wa wazalishaji wa teknolojia za nishati safi ya kupikia, kuandaa Mkakati wa Mawasiliano wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kubadilisha mitazamo ya wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi.

Pande hizo zimekubaliana kuendelea na majadiliano ya kitaalamu yatakayohusisha Wizara ya Nishati, Wizara ya Fedha, taasisi za fedha na wadau wengine muhimu ili kuandaa mpango wa pamoja wa kuharakisha upatikanaji wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa agenda ya nishati safi ya kupikia nchini.








No comments:

Post a Comment