Na. Josephine Majura, WF, Nairobi, Kenya.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Shelter Afrique Development Bank (ShafDB) pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 26 wa Wanahisa wa Taasisi ya Bima ya Biashara na Uwekezaji Afrika (ATIDI), unaoendelea jijini Nairobi, Kenya.
Mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo, hususan katika maeneo ya uwekezaji, maendeleo ya makazi na uhamasishaji wa rasilimali za kifedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pande zote mbili zilikubaliana kuendeleza ushirikiano wa kimkakati utakaongeza fursa za uwekezaji, upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya makazi na miundombinu inayohusiana na sekta hiyo, pamoja na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi.
Kwa upande wake, Serikali ya Tanzania ilieleza utayari wake wa kuendelea kushirikiana na ShafDB katika kubaini na kutumia fursa mbalimbali za maendeleo zitakazochangia kuimarisha upatikanaji wa makazi bora, kukuza sekta ya makazi na kuongeza ustahimilivu wa miundombinu, kwa kuzingatia sheria, taratibu na vipaumbele vya maendeleo vya Taifa.
Naye mwakilishi wa Shelter Afrique Development Bank (ShafDB) Bw. Charles Kazuka, alieleza utayari wa Benki hiyo kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika kufadhili miradi ya maendeleo ya makazi na miundombinu, akibainisha kuwa Tanzania itaendelea kuwa mshirika muhimu katika utekelezaji wa dhamira ya Benki ya kuchochea maendeleo endelevu barani Afrika.
Shelter Afrique Development Bank (ShafDB) ni taasisi ya kifedha ya kimataifa inayomilikiwa na nchi za Afrika pamoja na taasisi za fedha za maendeleo, ikiwa na dhamira ya kuhamasisha uwekezaji na kutoa ufadhili wa miradi ya makazi na miundombinu inayohusiana na sekta hiyo barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi waanzilishi wa Benki hiyo na imeendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli zake tangu ilipoanzishwa, hatua inayoendelea kuimarisha nafasi yake katika kuendeleza ushirikiano wa kikanda kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.
Katika mkutano huo Mhe. Munde, aliambatana na Kaimu Kamishna Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha, Wizara ya Fedha Bi. Dionisia Mjema na wataalamu kutoka Wizara hiyo.






No comments:
Post a Comment