Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), akisikiliza kwa makini wakati wa ufunguzi wa mkutano wa maazimio na mapendekezo yaliyofikiwa na vikao vya Makatibu Wakuu wa Hazina, wakati wa vikao vya SADC vinavyoendelea jijini Harare, Zimbabwe.
Na Eva Ngowi, Harare, Zimbabwe
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaofanyika jijini Harare, Zimbabwe, ambapo Tanzania imewasilisha msimamo wake kuhusu utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC (SADC Regional Development Fund) pamoja na mapendekezo ya vyanzo mbadala vya kugharamia miradi na programu za maendeleo za kikanda.
Akizungumza baada ya kikao hicho kilichowakutanisha Mawaziri wa Fedha, Magavana wa Benki Kuu na viongozi waandamizi wa sekta za fedha kutoka nchi 16 wanachama wa SADC, Mhe. Luswetula alisema pamoja na kujadili ajenda mbalimbali za maendeleo ya uchumi wa kikanda, Tanzania ilijielekeza katika masuala mawili yenye umuhimu wa kipekee kwa maslahi ya taifa.
Alieleza kuwa suala la kwanza lilihusu utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda wa SADC, ambapo Tanzania ilieleza kuwa iliridhia mkataba wa Mfuko huo mwaka 2016 na kwa sasa inaendelea kukamilisha taratibu za ndani zitakazoruhusu kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Aidha, Tanzania ilitoa msisitizo kuwa pamoja na kwamba Mfuko huo ni muhimu katika Ukanda wa SADC, hata hivyo bado kuna changamoto hususan ya upatikaji wa mtaji wa kuanzia kutoka kwa nchi wanachama kutokana na changamoto za kiuchumi walizonazo.
“Tumeeleza kuwa baada ya kukamilika kwa taratibu zote za ndani, Serikali itaijulisha rasmi Sekretarieti ya SADC ili Tanzania iweze kuanza kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo wa Kikanda,” alisema Mhe. Luswetula.
Alisema suala la pili lilihusu mapendekezo ya kutumia tozo za utalii (Tourism Levy) pamoja na ushuru wa forodha (Import levy) kama vyanzo vya kugharamia bajeti, miradi na programu za maendeleo za SADC, ambapo Tanzania ilieleza kuwa mapendekezo hayo yanahitaji kuangaliwa kwa kina zaidi.
Mhe. Luswetula alifafanua kuwa matumizi ya mapato yanayotokana na ushuru wa forodha kwa madhumuni hayo yanakinzana na mfumo wa usimamizi wa mapato nchini Tanzania, kwa kuwa Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya mwaka 2015, iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2023, inaelekeza kuwa mapato yote yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yaingizwe katika Mfuko Mkuu wa Serikali.
Aidha, alisema Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa matumizi ya tozo za utalii yanaweza kuongeza gharama za utalii nchini, jambo ambalo linaweza kupunguza ushindani wa sekta hiyo na kuathiri jitihada za kuvutia watalii wengi zaidi.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania ilipendekeza nchi wanachama ziongeze uwajibikaji kwa kuwasilisha michango yao kwa wakati na kuhakikisha nchi ambazo bado hazijatekeleza wajibu huo wa kimkataba zinatimiza ahadi zao, badala ya kuanzisha tozo mpya zitakazoweza kuathiri uchumi wa nchi wanachama.
“Tunaamini njia endelevu ni kuhakikisha kila nchi inatimiza wajibu wake wa kuchangia bajeti ya SADC kwa wakati ili kuwezesha utekelezaji wa miradi na programu za maendeleo ya kikanda,” alisema Mhe. Luswetula.
Mbali na masuala ya sera za fedha, Mhe. Luswetula alisema mkutano huo umeendelea kufungua fursa mpya za biashara na uwekezaji kwa nchi wanachama, huku akiwasihi wafanyabiashara wa Tanzania kutumia ipasavyo soko la SADC lenye nchi 16 na watu zaidi ya million 417 kwa kupanua biashara zao katika sekta mbalimbali, hususan kilimo, biashara na huduma.
Aidha, alibainisha kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha sekta ya utalii kwa kutumia fursa zilizopo ndani ya ukanda huo, akieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana kupitia kampeni ya Royal Tour iliyoanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yameongeza idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania.
“Kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, tutaendelea kuongeza nguvu katika kuitangaza Tanzania ili iwe kitovu cha utalii barani Afrika,” alisema Mhe.Luswetula.
Mkutano huo wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa SADC umejadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kifedha, uwekezaji, biashara na maendeleo ya kikanda, huku ukilenga kuimarisha ustahimilivu wa uchumi wa nchi wanachama na kuharakisha utekelezaji wa programu za maendeleo chini ya Ajenda ya Maendeleo ya Kikanda ya SADC.
Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Mwenyekiti wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa SADC ambaye pia ni Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Mhe. Enoch Godongwana; ambapo alizitaka nchi wanachama kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika kukabiliana na changamoto za uchumi wa dunia, kuendeleza vyanzo endelevu vya ufadhili wa maendeleo, pamoja na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati itakayochochea ukuaji wa uchumi, biashara na uwekezaji ndani ya ukanda wa SADC.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), (wa sita kulia) katika picha ya pamoja na Mawaziri wa Fedha na Magavana wa Benki Kuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), wakati wa vikaovinavyoendelea jijini Harare, Zimbabwe.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), (kulia), akifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano wa maazimio na mapendekezo wa Mawaziri wa Fedha, Uwekezaji na Afya. Kushoto ni Naibu Waziri Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya (Mb).
Ujumbe kutoka Tanzania ukifuatailia ufunguzi wa mkutano wa Mkutano wa Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC unaoendelea Harare nchini Zimbabwe.
Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), (kulia) akifurahia jambo wakati wakibadilishana Mawazo na Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe Mhe, CP Suzan Kaganda, (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani – WHO, Prof. Mohamed Yakub Janabi wakati wa mapumziko ya Vikao vya Mikutano ya Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inayoendelea Harare nchini Zimbabwe. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)

No comments:
Post a Comment