Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb.), leo Julai 27, 2026, ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 100, utakaotekelezwa katika eneo la Ngunga, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga.
Mkataba huo wenye thamani ya shilingi bilioni 204.7 umesainiwa kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mwakilishi wa mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni za Sagemcom Energy & Telecom SAS na STEG International Services.
Waziri Ndejembi amesema mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mseto wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme (Energy Mix), ikiwa ni utekelezaji wa azma ya kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, wa gharama nafuu na unaotokana na vyanzo vya nishati jadidifu.
Amefafanua kuwa, mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili zenye uwezo wa jumla wa kuzalisha Megawati 150. Awamu ya kwanza yenye uwezo wa Megawati 50 iligharimu shilingi bilioni 118.3 na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Aidha, Waziri Ndejembi amesema awamu ya pili yenye uwezo wa Megawati 100, ambayo utekelezaji wake umeanza rasmi kupitia utiaji saini wa mkataba utagharimu shilingi bilioni 204.7. Jumla ya gharama za utekelezaji wa awamu zote mbili ni shilingi bilioni 323.
Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vya nishati jadidifu, kuimarisha uthabiti wa mfumo wa umeme nchini na kuchangia kufikiwa kwa lengo la Serikali la kuwa na mseto wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme pamoja na kufikia uwezo wa kuzalisha umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Hafla hii imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba; Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita; Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba; Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, pamoja na viongozi wengine wa Serikali, Chama cha Mapinduzi na wadau wa sekta ya nishati.






No comments:
Post a Comment