OFISI YA WAZIRI MKUU YAWAWEZESHA WATU WENYE ULEMAVU KUNG'ARA MAONESHO YA SABASABA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, July 7, 2026

OFISI YA WAZIRI MKUU YAWAWEZESHA WATU WENYE ULEMAVU KUNG'ARA MAONESHO YA SABASABA


Na; Mwandishi Wetu - Dar es Salaam.


Ofisi ya Waziri Mkuu imewezesha watu wenye ulemavu nchini kushiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kupitia Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA).

Ushiriki huo umewawezesha kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa pamoja na kufanya biashara katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Akitembelea mabanda wakati wa maonesho hayo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga, ameoneshwa kuridhishwa na kiwango cha ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maonesho ya mwaka huu, akibainisha kuwa ushiriki huo umeongeza fursa za kiuchumi na kuwajengea kujiamini zaidi.

Mhe. Nderiananga alisema Serikali imegharimia ushiriki wa watu wenye ulemavu katika maonesho hayo bila wao kubeba gharama yoyote, hatua iliyowapa nafasi ya kutangaza bidhaa zao na kufanya biashara katika mazingira yenye usawa na heshima na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuboresha ushiriki huo katika miaka ijayo ili watu wengi zaidi wenye ulemavu wanufaike na fursa hizo.

Aidha, aliipongeza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) pamoja na Taasisi nyingine zilizowezesha ushiriki huo, huku akizitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutenga na kutoa mikopo ya asilimia mbili kwa watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kukuza shughuli zao za kiuchumi.

"Ni wakati sasa kwa watu wenye ulemavu kuendelea kuonesha uwezo wao katika uzalishaji na biashara. Kupitia maonesho haya tumejionea matokeo chanya ya uwezeshaji wa kiuchumi unaotokana na mikopo na fursa zinazotolewa na Serikali". alisema Mhe. Nderiananga.

Kwa upande wake, mwakilishi wa washiriki hao, Bi. Pili Bilahi, aliishukuru Serikali kwa kuwawezesha kushiriki katika maonesho hayo bila kulipia gharama yeyote.

Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi yanayowapa watu wenye ulemavu fursa za kiuchumi, ikiwemo kupitia mikopo ya asilimia mbili ya mapato ya ndani inayotolewa na halmashauri kwa watu wenye ulemavu.

Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere chini ya kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba ni Fahari ya Tanzania," yakilenga kukuza biashara, uwekezaji na ubunifu nchini.

No comments:

Post a Comment