SERIKALI KUENDELEA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, July 24, 2026

SERIKALI KUENDELEA KUFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI


Na Mwandishi Wetu - 
MWANZA


Kamishna wa Madini nchini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, amesema Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zinazoikabili Sekta ya Madini kwa kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji ili kuongeza uzalishaji, mapato ya Serikali kuongezeka na mchango wa sekta hiyo kuendelea kukua katika uchumi wa Taifa.

Dkt. Mwanga ameyasema hayo mapema leo Julai 24, 2026, wakati akifunga Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF 2026), lililofanyika jijini Mwanza kuanzia Julai 22 hadi 24, mwaka huu.

Amesema Serikali imeweka mikakati ya kujenga Sekta imara ya Madini kwa kufungua fursa zaidi za uwekezaji na kuendelea kutafuta suluhisho la changamoto za mitaji na teknolojia zinazowakabili wadau, hatua inayolenga kuongeza tija na kuhakikisha Sekta ya Madini inakuwa nguzo muhimu ya uchumi wa nchi.

“Sekta ya Madini ni miongoni mwa sekta muhimu zilizopewa kipaumbele katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Wizara ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ya kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa kuboresha sheria na kanuni, kwa kushirikiana na wadau ambao ni muhimu sana,” amesema Dkt. Mwanga.

Amesema kupitia majukwaa mbalimbali, Wizara ya Madini imekuwa ikipokea mrejesho na mapendekezo kutoka kwa wadau wa sekta hiyo, ambayo yamekuwa yakisaidia katika kuboresha sheria, kanuni na mifumo ya usimamizi wa sekta hiyo.

Dkt. Mwanga amesema ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini una manufaa makubwa kwa wananchi na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuanzia katika shughuli za uchimbaji, uchenjuaji hadi biashara ya madini.

Ametoa wito kwa wadau wa Sekta ya Madini kuendelea kushirikiana na Serikali kwa uadilifu na uwazi, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha Watanzania wanapata elimu na kunufaika kikamilifu na fursa zinazotokana na shughuli za madini nchini.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Madini itafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na wadau katika jukwaa hilo, kama ilivyo utaratibu wa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwanga amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake ya kuipa kipaumbele Sekta ya Madini, ambayo amesema imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na ni miongoni mwa sekta zinazotarajiwa kuwa na nafasi muhimu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Pia ameupongeza uongozi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, wadau wa Sekta ya Madini na wataalam kutoka Tume ya Madini kwa kufanikisha jukwaa hilo kwa usalama na kwa kiwango cha juu, pamoja na kushirikishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa ushirikishwaji wa wazawa katika Sekta ya Madini.
Wakati huohuo, Kamishna wa Tume ya Madini, Mhandisi Theonestina Mwasha, amesema Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini limekuwa na manufaa makubwa kwa wamiliki wa leseni, wataalam wa ushirikishwaji wa Watanzania, watoa huduma, taasisi za Serikali na binafsi, pamoja na vyama vya wachimbaji wa madini.

Mhandisi Mwasha amesema washiriki wa jukwaa hilo wamepata fursa ya kubadilishana mawazo, kujadili changamoto na kupata uzoefu kutoka kwa washiriki wengine, hususan wataalam kutoka Ghana, katika namna bora ya kuimarisha ushirikishwaji wa wazawa katika Sekta ya Madini.

Kabla ya kufunga jukwaa hilo, Dkt. Mwanga ametembelea maonesho yaliyokuwa yakifanyika katika eneo la jukwaa na kutoa tuzo kwa wadhamini waliowezesha kufanyika kwa Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini.

No comments:

Post a Comment