Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema kazi ya ujenzi wa barabara inayoendelea nchini kote ina lengo la kuifungua Tanzania kwa kuiunganisha na jirani zake.
Akizungumza katika maeneo tofauti mkoani Kagera wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara inayoendelea mkoani humo, Ulega alisema lengo la Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba hakuna eneo linaloachwa nyuma kimaendeleo kwa sababu ya kutofikika.
“ Naomba niwaeleze leo kwamba tunajenga barabara hizi ili kuhakikisha kwamba hakuna mkoa au eneo linaachwa nyuma kwa sababu halijaunganishwa na wengine. Na tunaposema wengine hatumaanishi Watanzania tu bali na majirani zetu pia,” alisema.
Waziri huyo aliyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Rusahunga – Rusumo ambayo inaunganisha Tanzania na nchi za Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Ujenzi wa barabara hiyo ulioanza Julai 2023, umeigharimu serikali kiasi cha shilingi bilioni 210 na ujenzi wake sasa umefikia asilimia 73. 9.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika tukio hilo, baadhi ya wananchi na viongozi mkoani Kagera walisema ujenzi wa barabara hiyo utapunguza kero, usumbufu na muda wa kusafiri uliokuwa ukitumika katika siku za nyuma.
Mbunge wa Ngara, Doto Bahemu, alikumbusha namna alivyowahi kulala barabarani baada ya gari lake kupasuka matairi usiku wakati akielekea kijijini kwake kutokana na ubovu wa barabara.
“Binafsi sina maneno ya kutosha kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa barabara hii. Zamani mtu ukitoka Dar kuja Ngara ulikuwa ukifika hapa Rusahunga ndiyo inakuwa kama umeanza safari upya. Tunaishuru sana serikali kwa barabara hii,” alisema.









No comments:
Post a Comment