LONDO AWATAKA MAAFISA BIASHARA KUFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI NCHINI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 17, 2026

LONDO AWATAKA MAAFISA BIASHARA KUFUNGUA MILANGO YA UWEKEZAJI NCHINI


NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo,akizungumza wakati wa Mkutano wa Tatu Kati ya Wizara na Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda,Biashara na Uwekezaji katika Sekretariet za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika kuanzia leo Agosti 17 hadi 18 jijini Dodoma.


Na Okuly Julius, OKULY BLOG – Dodoma


Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amewataka Maafisa Biashara nchini kutumia nafasi zao kuibua fursa za uwekezaji, kuongeza thamani ya mazao na kuboresha mazingira ya biashara katika halmashauri ili kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Londo ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano wa Tatu Kati ya Wizara na Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda,Biashara na Uwekezaji katika Sekretariet za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kinachofanyika kuanzia leo Agosti 17 hadi 18 jijini Dodoma,kilicholenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya maafisa hao katika kukuza biashara, viwanda na uwekezaji nchini.

Amesema Maafisa Biashara wana nafasi muhimu katika kutambua fursa zilizopo katika maeneo yao na kuwaunganisha wafanyabiashara, wawekezaji na Serikali ili kuongeza uzalishaji, ajira na mchango wa sekta ya viwanda katika uchumi wa Taifa.

Kwa mujibu wa Londo, utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau mbalimbali, ikiwemo Maafisa Biashara ambao wako karibu na wafanyabiashara na shughuli za kiuchumi katika ngazi za halmashauri.

Amesema Dira hiyo ina malengo makubwa ya kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa viwanda katika Afrika Mashariki na Kati, huku ikilenga kufikia uchumi wa dola trilioni moja na kuongeza kipato cha Mtanzania hadi dola 7,000.

Amewataka Maafisa Biashara kuhakikisha wanatumia taarifa na takwimu za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao kutambua sekta zenye fursa za uwekezaji na kuzifikisha kwa wawekezaji na wadau wengine.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa, amesema kuna umuhimu wa kuboresha muunganiko wa mifumo ya kidijitali ili kurahisisha usajili wa biashara na utoaji wa leseni kupitia mfumo mmoja.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza urasimu, kuokoa muda na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara, sambamba na kuongeza ufanisi katika mazingira ya biashara nchini.

Kikao hicho pia kimewakutanisha viongozi na wataalamu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Maafisa Biashara wa Mikoa kwa lengo la kujadili namna bora ya kutekeleza majukumu yao na kuchochea maendeleo ya biashara, viwanda na uwekezaji.

Katika hatua nyingine, Wakala wa Vipimo (WMA) umeahidi kuimarisha ushirikiano na Maafisa Biashara wa Mikoa katika kuhakikisha shughuli za biashara zinaendeshwa kwa kuzingatia matumizi ya vipimo sahihi, huku haki na maslahi ya mlaji yakilindwa.

Meneja wa Sehemu ya Ukaguzi na Ufuatiliaji wa WMA, Jadi Athumani Kijumu, amesema ushirikiano huo ni muhimu kutokana na nafasi ya Maafisa Biashara kuwa kiungo kati ya WMA, wafanyabiashara na Serikali za Mikoa.

Amesema kupitia ushirikiano huo, WMA itaweza kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi na ufuatiliaji wa vipimo, pamoja na kupata taarifa sahihi kuhusu wafanyabiashara na maeneo wanayofanyia shughuli zao.

“Maafisa Biashara ni kiungo muhimu kati yetu na wafanyabiashara waliopo katika mikoa. Ushirikiano wao utatusaidia kuwafahamu wafanyabiashara na maeneo wanayofanyia biashara ili kurahisisha huduma za ukaguzi na ufuatiliaji,” amesema Kijumu.

Amesema WMA imetumia kikao hicho kutoa elimu kwa Maafisa Biashara kuhusu majukumu ya Wakala na namna wanavyoweza kushirikiana katika kutatua changamoto zinazohusu matumizi ya vipimo, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za watumiaji.
Kijumu amesema ushirikiano huo pia utasaidia kuimarisha utendaji wa Kamati za Ushauri za Mikoa, ambazo WMA na Maafisa Biashara ni wajumbe, kwa kuwezesha kero na malalamiko ya wafanyabiashara kushughulikiwa kwa wakati.

Ameongeza kuwa WMA inataka wafanyabiashara kuhakikisha wanatumia vipimo vilivyokaguliwa na kuthibitishwa kuwa sahihi ili kuzuia ukiukwaji wa haki za watumiaji na kuongeza uaminifu katika shughuli za biashara.

Ushirikiano kati ya Wizara, WMA, BRELA na Maafisa Biashara unatarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa biashara, kuboresha mazingira ya uwekezaji, kulinda haki za mlaji na kuongeza mchango wa biashara na viwanda katika uchumi wa Taifa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.





No comments:

Post a Comment