MATI TECHNOLOGIES YAONYESHA UWEZO WA WATANZANIA KATIKA TEKNOLOJIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 6, 2026

MATI TECHNOLOGIES YAONYESHA UWEZO WA WATANZANIA KATIKA TEKNOLOJIA

 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mizengo Pinda, ameshangazwa na kiwango cha ubunifu wa teknolojia zinazobuniwa na kuzalishwa na kampuni ya Mati Technologies baada ya kutembelea banda la kampuni hiyo katika Maonesho ya 33 ya Kitaifa ya Kilimo (Nane Nane 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.

Mhe. Pinda alitembelea banda hilo leo na kupokea maelezo kutoka kwa viongozi na wataalamu wa Mati Technologies kuhusu shughuli mbalimbali zinazofanywa na kampuni hiyo katika kubuni na kutengeneza teknolojia zinazolenga kuongeza tija katika sekta ya kilimo na maeneo mengine ya maendeleo.

Katika ziara hiyo, alikagua teknolojia mbalimbali zinazotengenezwa na kampuni hiyo, ikiwemo ndege nyuki zinazotumika kunyunyiza viuatilifu na mbolea mashambani kwa usahihi, haraka na ufanisi mkubwa, pamoja na mifumo mingine ya kisasa ya kiteknolojia inayolenga kuboresha uzalishaji wa kilimo.

Baada ya kushuhudia namna teknolojia hizo zinavyofanya kazi, Mhe. Pinda alisema ameridhishwa na hatua kubwa ya ubunifu iliyofikiwa na wataalamu wa Kitanzania.



“Ni jambo la kujivunia kuona Watanzania wakibuni na kuzalisha teknolojia za kisasa zinazotoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali za maendeleo, hususan katika sekta ya kilimo,” alisema.

Alisema maendeleo hayo yanaonesha uwezo mkubwa wa wataalamu wa ndani katika kubuni teknolojia zinazokidhi mahitaji ya nchi na kuchangia kukuza uchumi kupitia sekta ya kilimo na viwanda.


Aidha, aliipongeza Mati Technologies kwa kuwekeza katika utafiti, ubunifu na uzalishaji wa teknolojia za ndani, akisisitiza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono ili kuharakisha maendeleo ya taifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Kitanzania katika soko la ndani na kimataifa.

Kwa upande wake, uongozi wa Mati Technologies ulisema kampuni itaendelea kubuni na kuzalisha teknolojia zenye ubora wa hali ya juu zitakazorahisisha shughuli za uzalishaji, kuongeza tija kwa wakulima na kuchochea matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali za uchumi.





Maonesho ya Nane Nane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kuonesha mafanikio ya sekta za kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na teknolojia, huku yakivutia maelfu ya wananchi, wakulima, wawekezaji, wanafunzi na wataalamu kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kupitia ubunifu wa teknolojia zinazozalishwa hapa nchini, Mati Technologies inaendelea kujijengea sifa kama moja ya kampuni zinazochochea matumizi ya sayansi, teknolojia na utafiti katika kuongeza tija ya uzalishaji na kuchangia maendeleo endelevu ya Tanzania.





No comments:

Post a Comment