Na.WMJJWM - Dodoma
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju amesema Jukwaa la wanawake katika sekta ya ushirika ni nyezo muhimu katika kujenga uchumi wa familia, Jamii na Taifa kupitia sekta hiyo.
Mpanju ameyasema hayo wakati akifungua Jukwaa hilo linaloundwa na shirikisho la vyama vya ushirika Tanzania (TFC), lililofanyika Agosti 06, 2026 sambamba na maonesho ya Wakulima Nanenane kwenye Viwanja vya John Malecela, Nzunguni Jijini Dodoma.
"Maendeleo hayawezi kuwa kamili wala endelevu kama wanawake wataachwa nyuma. Taifa lolote linalowekeza kwa wanawake huwekeza katika ustawi wa familia, Jamii na Taifa kwa ujumla" amesema Mpanju.
Amesema pia, katika kufikia Dira 2050, sekta ya ushirika ina nafasi ya kipekee ya kuhakikisha wanawake wanapata fursa sawa za kumiliki rasilimali, kupata masoko, mitaji, elimu, teknolojia na kushiriki kikamilifu katika maamuzi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa hilo Taifa Pili Marwa, amebainisha kuwa, Jukwaa hilo limewakutanisha jumla ya wanawake 460 kutoka Tanzania Bara na Visiwani, ambapo limekuwa fursa kwa washiriki hao kubadilishana uzoefu katika utafutaji wa mitaji, mikopo na soko la mazao ndani na nje ya nchi.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kuendelea kuratibu majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi nchini, ili kuhakikisha wanakuwa na uwezo wa kuongeza kipato kwa shughuli za ujasiriamili, biashara na uzalishaji, ubunifu na Uwekezaji.
Jukwaa hilo linaongozwa na kaulimbiu isemayo "Ushirika kwa Maendeleo Jumuishi: Usimwache Mwanamke Nyuma." ambayo inaakisi moja kwa moja malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza kujenga jamii jumuishi na uchumi shindani.









No comments:
Post a Comment