Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, amekitaka Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kuwa wabunifu na kujikita katika utekelezaji wa majukumu yao ya msingi, akisisitiza kuwa wananchi na Taifa wanawategemea katika kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Uongozi mpya wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), walipomtembelea na kujitambulisha rasmi, tarehe 4 Agosti, 2026, Ofisi Ndogo ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Mhe. Johari amesema TPBA kina wajibu mkubwa wa kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku akisisitiza umuhimu wa kutoa ufafanuzi kuhusu upotoshaji unaofanyika katika mitandao ya kijamii, akieleza kuwa bila kufanya hivyo, jamii inaweza kufanya maamuzi kutokana na taarifa zisizo sahihi.
Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA), *Bw. Bonaventure Pardon Mwambaja,* ameahidi kuwa uongozi wake utatekeleza kwa vitendo mpango kazi uliowekwa ili kuhakikisha chama kinaendelea kutoa huduma bora kwa Taifa.
Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kililenga kuutambulisha rasmi uongozi mpya wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kwa mlezi wao, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari, pamoja na kuwasilisha mpango kazi wao wa utekelezaji wa majukumu ya Chama.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali aliambatana na Viongozi wengine wa Chama hicho akiwemo Makamu wa Rais, Bw. Acley Chaule, Mwenyekiti Bi. Selestina Kunambi, na Makamu Mwenyekiti Bi. Farida Kiobya.








No comments:
Post a Comment