WAZIRI MKUU ASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 4, 2026

WAZIRI MKUU ASISITIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KATIKA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI.


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesisitiza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo, mifugo na uvuvi kwa lengo la kuongeza tija, kupunguza gharama za uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

"Jitihada zinazofanywa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zinapaswa kuendelezwa kwa kutumia teknolojia na ubunifu ili kukuza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla," amesema Waziri Mkuu.

Dkt. Mwigulu ametoa wito huo mkoani Morogoro, leo (Jumane Agosti 4, 2026) alipotembelea maonesho ya Wakulima, Wavuvi na Wafugaji (Nanenane) Kanda ya Mashariki, yanayofanyika mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ametembelea mabanda mbalimbali ya maonesho, likiwemo Banda la Bodi ya Sukari Tanzania, ambako alijionea matumizi ya teknolojia ya ndege isiyo na rubani (drone) aina ya DJI AGRAS T50 inayotumika katika umwagiliaji na usambazaji wa mbolea kwenye mashamba ya miwa.

"Matumizi ya teknolojia hii yanapaswa kupewa kipaumbele katika sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao, hususan miwa, na kuchangia upatikanaji wa sukari ya kutosha nchini."

"Ni teknolojia inayorahisisha mambo, itawafanya hata vijana wavutiwe na kilimo," amesisitiza Dkt. Mwigulu.

Waziri Mkuu amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza uwekezaji katika sekta ya kilimo na kuwezesha kuimarishwa kwa tafiti, matumizi ya teknolojia za kisasa na ongezeko la uzalishaji wenye tija kwa maendeleo ya Taifa.

Akiwa katika banda la Jeshi la Magereza pamoja na Banda la Halmashauri ya Jiji la Tanga, ambako amejionea mifumo ya kisasa ya ufugaji wa ng’ombe na wanyama wengine, Waziri Mkuu amesisitiza kuwa ufugaji wa kisasa ni muhimu katika kuongeza tija, kuboresha kipato cha wafugaji na kupunguza migogoro kati ya wakulima, wafugaji na wawekezaji.

Akizungumza na viongozi baada ya kutembelea mabanda hayo, Waziri Mkuu amesema maonesho ya Nanenane si jukwaa la kuonesha bidhaa pekee, bali ni sehemu ya kuonesha utekelezaji wa shughuli halisi zinazofanywa na Watanzania katika maeneo yao.

"Maonesho yanafurahisha kwa kiasi kikubwa sana, na tutakapofikia mafanikio haya makubwa sana tunayoyaona kwenye maonesho, kwamba ndiyo _standard_ ya maisha, ni hatua kubwa na nzuri, tutakapofikia hapo kwa kweli lengo la kufikia wastani wa pato la kila mtu haitakuwa tu wastani, itakuwa ni pato halisi," ameongeza Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesisitiza matumizi ya nishati safi, hususan gesi asilia katika shughuli za kilimo na umwagiliaji ili kupunguza gharama za uzalishaji zinazotokana na matumizi ya mafuta. Ambapo ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuboresha na kusambaza huduma ya nishati hiyo katika maeneo mbalimbali ili kuongeza ufanisi katika uzalishaji.

Vilevile, Waziri Mkuu alielekeza kuongezwa kwa uzalishaji wa mbegu bora za mazao, vifaranga bora pamoja na kuimarishwa kwa huduma za ugani ili kuongeza tija, kuboresha ubora wa mazao na bidhaa za mifugo na uvuvi, na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kadhalika, alielekeza sekta ya kilimo kuweka mkazo katika uhifadhi bora wa mazao baada ya mavuno ili kupunguza upotevu na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa huku akiwahimiza vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo, akisema kilimo si shughuli ya wazee pekee bali ni eneo lenye fursa kubwa za ajira, ubunifu na maendeleo ya kiuchumi.

No comments:

Post a Comment