NCHIMBI AIPONGEZA TADB KWA KUCHOCHEA MAENDELEO YA KILIMO NA UJASIRIAMALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 3, 2026

NCHIMBI AIPONGEZA TADB KWA KUCHOCHEA MAENDELEO YA KILIMO NA UJASIRIAMALI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, ameipongeza Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali, akisisitiza kuwa juhudi hizo zina mchango muhimu katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Dkt. Nchimbi amesema hayo leo, Agosti 3, 2026, alipotembelea banda la TADB katika Viwanja vya Dkt. John Samuel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma, kunakoendelea Maonesho ya 33 ya Kitaifa na Kimataifa ya Nanenane 2026.

Akiwa katika banda hilo, Makamu wa Rais alipata maelezo kuhusu programu mbalimbali zinazotekelezwa na TADB za kuwezesha sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia huduma za kifedha, ambapo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau wote katika kuharakisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Maonesho ya mwaka huu yanafanyika chini ya lengo la kuongeza tija katika sekta ya kilimo na kuhamasisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kupitia ushiriki wa taasisi za umma na binafsi.

Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa Serikali imeendelea kuiimarisha TADB kwa kuongeza mtaji wake kutoka shilingi bilioni 60 hadi zaidi ya shilingi bilioni 400, hatua iliyowezesha benki hiyo kupanua uwezo wake wa kutoa mikopo na huduma za kifedha kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali nchini.

No comments:

Post a Comment