Dodoma.
Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) limesema ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane Kitaifa unalenga kutangaza bidhaa zinazozalishwa na shirika hilo pamoja na kuwaelimisha wananchi kuhusu majukumu yake katika kuendeleza sekta ya madini nchini.
Afisa Masoko wa STAMICO, Beatus Nzogela, amesema shirika hilo pia linatumia maonesho hayo kuwaonesha wananchi mchango wake katika kuwawezesha wachimbaji wadogo wa madini kupitia utoaji wa mitambo ya kisasa ya uchimbaji.
Amesema kwa sasa STAMICO ina mitambo 14 inayotolewa kwa wachimbaji wadogo, hatua ambayo imewawezesha wengi wao kuongeza tija na kuimarisha shughuli zao za uchimbaji.
Mbali na huduma hizo, Nzogela amesema STAMICO inazalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes, ambao umeendelea kupata mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi kutokana na ubora na faida zake katika matumizi ya nishati.
Aidha, amesema shirika hilo linasimamia pia Kiwanda cha Chumvi kilichopo mkoani Lindi pamoja na Kiwanda cha Karasha kinachozalisha kokoto katika eneo la Chigongwe, jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Nzogela, banda la STAMICO limeendelea kuvutia idadi kubwa ya wananchi na viongozi mbalimbali wanaotembelea maonesho hayo, huku baadhi yao wakionesha nia ya kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na shirika hilo.
Amebainisha kuwa viongozi wa Bodi ya Tumbaku Tanzania wameomba kukutana na Menejimenti ya STAMICO ili kujadili uwezekano wa kutumia nishati ya Rafiki Briquettes katika viwanda vya kukaushia tumbaku na vile vya kuzalisha mafuta ya mawese.
"Mapokezi ni makubwa sana. Tunafurahishwa na mwitikio wa wananchi pamoja na taasisi mbalimbali zinazotembelea banda letu na kuona fursa zilizopo," amesema.
Nzogela ametoa wito kwa wananchi wote wanaotembelea Maonesho ya Nanenane kufika katika banda la STAMICO ili kujionea bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na shirika hilo pamoja na kupata elimu kuhusu shughuli zake.

No comments:
Post a Comment